Mrema amfananisha Rais Magufuli na Baba wa Taifa, Julius Nyerere

2274
0
Share:

Aliyekuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na mwenyekiti wa Parole, Augustine Mrema amemfananisha Rais John Pombe Magufuli na Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika utendaji kazi wake.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii Lyatonga alisema kuwa utendaji kazi wa Rais Magufuli hautofautiani na ule wa wa Baba wa Taifa kwani wote wanachukia rushwa, ufisadi na kujilimbikizia mali kwa viongozi wa serikali.

“Mwalimu Nyerere alichukia sana rushwa na alichukua hatua kali sana kwa wala rushwa wote bila kujali nyadhifa zao au uwezo wao wa kifedha, nakumbuka kuna waziri wake mmoja alihukumiwa kifungo na viboko baada ya kupatikana na hatia ya kula rushwa,” alisema Lyatonga.

Aliongeza kuwa Watumishi wote wa umma, waliohusika na ufisadi walichukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufungwa jela na kufilisiwa mali zao nakupelekea kupunguza sana rushwa na ufusadi serikalini.

“Mwalimu Nyerere alileta Azimio la Arusha ambalo lilizuia viongozi kujilimbikizia mali na alitenganisha siasa na biashara ambapo wanasiasa hawakuruhusiwa kufanya biashara na wafanyabiashara hawakuruhusiwa kushika nafasi za uongozi kitendo ambacho Dkt. Magufuli anafuata nyayo zake,” alisema Lyatonga.

Mrema aliongeza kuwa Viongozi wa leo wanapaswa kujifunza kutoka kwa Mwalimu Nyerere kwani Mwalimu alikuwa muadilifu, hakujilimbikizia mali, na wala hakuwahi kutumia madaraka yake kwa manufaa yake binafsi ndiyo maana
hata watoto wake walisoma shule ndani ya nchi yetu kwenye shule za kawaida.

Na. Eliphace Marwa – Maelezo.

Share:

Leave a reply