MSD yaeleza mikakati yake, dawa zipo bwelele nchini

529
0
Share:

Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) kupitia kwa Mkurugenzi wake Bw. Laurean Bwanakunu amebainisha kuwa, kwa sasa na kipindi kingine dawa zipo bwelele na za kutosha  baada ya kuboresha mambo mbalimbali ikiwemo Serikali kutenga bajeti kubwa yenye kukidhi kasi ya uingizaji wa dawa hapa nchini.

Bwanakunu amesema hali ya upatikanaji wa dawa kwasasa imeboreshwa kutoka asilimia 54 iliyokuwepo mwaka jana, hadi kufikia asilimia 74 hivi sasa  na kuhuhakikishia umma kuwa upatikanaji wa dawa utaimarika mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu hadi kufikia asilimia 90.

Amesema kwa sasa kati ya aina za dawa muhimu 135 zinazohitajika kuwepo MSD dawa aina 100 zinapatika kwenye maghala ya MSD.

Bwanakunu ameeleza kuwa, MSD imefanikiwa kurejesha Maghala iliyokuwa imekodi kwa ajili ya kuhifadhia vifaa tiba, hatua ambayo inaokoa sh.Bilioni 4 ambazo zilikuwa zikilipwa kama kodi kila mwaka.

Ameongeza kuwa, tayari wamekabidhiwa kiwanja eneo la Luguruni, wilayani Ubungo walichopewa na Rais John Magufuli ambacho kitatumika kujenga ofisi za Kanda ya Dar es Salaam.

Kuhusu maduka, ameeleza kuwa wiki ijayo wanatarajia kuzindua  duka la dawa la MSD mkoani Katavi, ambalo litaifanya MSD kuwa na jumla ya maduka Saba, mengine yakiwa mkoani Arusha, Dar es Salaam, Mwanza, Lindi, Geita na Mbeya.

Katika hatua nyingine  Bwanakunu amesema kuwa, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu anaangalia namna ya kuwawezesha akina mama wasio kuwa na uwezo wakununua vifaa maalum vya kujifungulia akina mama (kit) ambayo MSD wanatarajia kuvitoa.

Aidha, kwa sasa MSD inanunua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji, ilikuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba unakuwaendelevu na kupunguza gharama za ununuzi wa dawa hizo, ambazo asilimia 80 zinatoka nje ya nchi.

Afisa Mwandamizi wa Idara Habari Maelezo, Zamaradi Kawawa akifungua mkutano na waandishi wa Habari wakati wa kumkaribisha Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa (MSD) Laurean Bwanakunu (katikati). Kushoto ni Afisa Mkuu wa Mahusiano wa MSD, Etty Kusiluka.

Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa (MSD) Laurean Bwanakunu akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo pichani) leo  9 Januari 2017, wakati wa tukio hilo la kuelezea mipango ya Bohari ya dawa na mikakati yao.

Share:

Leave a reply