Mufti Mkuu ataka Kamati ya Taifa ya Amani ianzishwe

77
0
Share:

Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zubeir ameitaka serikali kuanzisha Kamati ya Taifa ya Amani, ili kuhamasisha utunzaji wa amani kwa wananchi.

Sheikh Zubeir ametoa wito huo leo Aprili 16, 2018 wakati akitoa salamu zake kwa viongozi wa dini mbalimbali waliohudhuria Mkutano wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam.

“Nishauri jambo moja kwamba kamati tuliyonayo ni ya mkoa, na ni mda mrefu tangu ianzishwe na kazi zake ni kubwa sana na imefanya kazi za kueleweka, na imekusanya dini zote, kuonesha kwamba amani ni ya watu wote, sasa ifikie katika ngazi ya taifa, tufikie katika kamati ya taifa ili tuwe na mtiririko mzuri, kuanzia taifa, mkoa, wilaya na kata,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa amesema tangu kamati hiyo ilipoundwa mwaka 2011 imefanya matukio mbalimbali ya kuimarisha mahusiano mema kwa jamii, ikiwemo kuandaa dua ya kuliombea Taifa.

“Kamati iliundwa tangu 2011, imefanya mambo mbalimbali kuleta mahusiano ikiwemo kuandaa mechi ya mpira wa miguu, tulicheza kwa kushirikiana, hatuna sababu ya kujenga chuki tunahitaji kuishi pamoja, kamati pia iliandaa dua maalumu ya kuliombea taifa 2015 mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan. kamati inaendelea kuunda kamati za wilaya za mkoa, tunaamini mikoa mingine itaunda kamati ya wilaya,” amesema.

Share:

Leave a reply