Muhimbili yapunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje

344
0
Share:

HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imeanza kutekeleza adhma ya Serikali ya kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje kwa vitendo ambao walikuwa wakifuata matibabu yasiyopatikana hapa nchini ama kutokana na kutokuwepo wataalamu au ukosefu wa vifaa vya kutolea huduma husika ili kuweza kupunguza gharama  kwa asilimia zaidi ya 50.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma Hospitalini hapo Bw. Aminiel Aligaesha (pichani) katika mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya hospitali kwa kipindi cha mwaka mmoja wa awamu ya Tano ya utawala wa Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

“Katika kutekeleza adhma ya Serikali ya awamu ya tano utawala wa Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Joseph Magufuli tumefanikiwa kupunguza wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje na kufanikiwa kuokoa gharama zaidi ya asilimia 50 kwa mwaka” alisema Aligaesha.

Aidha Bw. Aligaesha amesema kuwa katika kutekeleza hilo, Septemba 25, 2016, Hospitali hiyo  ilipeleka watalaamu saba nchini India katika Hospitali ya Apollo iliyopo New Delhi ili wakajifunze kwa njia ya vitendo jinsi ya kufanya upasuaji na upandikizaji wa kifaa cha usikivu kwa watu wazima na watoto il kuweza kuokoa shilingi milioni 80 hadi 100 kwa kila mgonjwa atakayepelekwa nje.

Bw. Aligaesha alisema kuwa Takwimu za MNH zinaonyesha kuwa asilimia 95 ya wagonjwa ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji wa kuwekewa kifaa cha usikivu ni watoto wadogo na kusisitiza kuwa huduma hii itasaidia watoto wengi hapa nchini na pia kujenga uwezo kwa wataalamu wa ndani ya nchi. 

Mbali na hayo Bw. Aligaesha amesema kuwa wagonjwa wanaokwenda nje kupata huduma za upandikizaji wa figo ambapo ifikapo mwanzoni mwa mwaka 2017 Hospitali itaweza kupandikiza figo hapa hapa nchini na kupanua huduma za kusafisha figo kutoka uwezo wa kuwa na mashine 23 hadi mashine 50 na pia kuongeza awamu za kuchuja figo kutoka mbili za sasa mpaka kufikia 3.

Aidha Hospitali ya Taifa Muhimbili imepeleka nchini India wataalamu 18 wa fani mbalimbali kwa ajili ya kujengewa uwezo wa upandikizaji figo kwa watu wenye matatizo ya figo na timu hiyo inatarajia kurejea mwishoni mwaka na kuanza kazi mara moja  ambapo huduma hiyo itsaidia kuokoa kiasi cha shilingi milioni 40 hadi 60 kwa mgonjwa mmoja .

”Uwepo wa huduma hizi hapa nchini utawezesha Watanzania wengi kupata huduma hii na kwa gharama nafuu zaidi hapa nchini na kupunguza mzigo kwa Serikali wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwani gharama za matibabu zitapungua kwa zaidi ya asilimia 50 hadi 60” alisema Bw. Aligaesha.

Na Ally Daud-MAELEZO

Share:

Leave a reply