Mulamu Erick Nghambi azindua rasmi kampeni zake za kuwania Umakamu wa Rais TFF

294
0
Share:

Leo Agosti 7,2017, Mgombea nafasi  ya Makamu wa Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF), Mulamu Erick Nghambi amejitokeza mbele ya vyombo vya habari na kuzindua rasmi mbio za kuwania nafasi hiyo ya Umakamu wa TFF.

“Nachukua nafasi hii kuwashukuru Wanahabari na wadau wote kutenga muda wenu na kuja kunipa heshima ya kuja kunisikiliza dhamira yangu kuelekea uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Leo ni siku yangu ya kuzindua kampeni zangu kuelekea uchaguzi mkuu wa TFF, hivyo nimeona ni vyema kuwaita hapa wanahabari niweke wazi dhamira na malengo yangu kuelekea katika uchaguzi huu muhimu” ameeleza Bwana Mulamuu Nghambi mapema leo Jijini Dar e Salaam.

Bwana  Mulamu Nghambi ameongeza kuwa, endapo atapata nafasi hiyo ya Umakamu wa Urais wa TFF, anaahidi  kuitendea haki kutokana na uzoefu alio nao kwa kutumia nyadhifa mbalimbali katika soka la Tanzania.

Miongoni wa mwa sifa za uzoefu wake ni pamoja na  kuwa na uzoefu  wa miaka 18 katika soka akiwa amepitia nafasi mbalimbali katika uongozi wake.  Amewahi kucheza  soka kwenye mashindano ya Umisseta akiwakilisha timu ya sekondari ya Agha Khan Mzizima na Mkoa wa Dar es salaam. Alicheza pia timu za Cosby FC, Seaview Rangers FC zote za Upanga na Oysterbay FC, zote hizo zilikuwa zikicheza soka la mtaani.

Kuanzia mwaka 2001 hadi sasa ni Katibu wa kundi la Friends of Simba linalosifika ndani ya klabu hiyo. Mwaka 2004 alichaguliwa kuwa Meneja Msaidizi klabu ya Simba na mwaka mmoja baadaye alikuwa Mtunza Fedha wa muda Simba.

Mwaka 2006 alikuwa Mjumbe kamati ya Usajili Simba, na 2008 Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Chama Cha Soka Dodoma (DOREFA) nafasi aliyodumu nayo kwa miaka nane.

Mwaka 2013 aliteuliwa kuwa Mjumbe kamati ya Kutengeneza Mpango Mkakati wa Klabu ya Simba wakati mwaka 2015 aliteuliwa tena kuwa Mjumbe wa Kamati Maalum ya Ushindi TFF.

Wasifu wa Mulamu ni mpana kwani 2014 aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Vijana ya TFF kabla ya mwaka 2016 kuteuliwa kuwa Mjumbe Kamati ya Mabadiliko Simba mwaka ambao pia aligombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Dodoma na kushinda.

Katika kuimalisha ushirikiano, Mulamu amebainisha kuwa, suala la kwanza endapo atachaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa TFF, yupo tayari kushirikiana bega kwa bega  na viongozi wengine ambao watachaguliwa ambao ni Rais pamoja na Wajumbe wa Kamati tendaji ili kuweza kuendesha sokka la Tanzania kutoka hapa lilipo na kulipeleka hatua nyingine.

“Mipango ya muda mfupi ni pamoja na kusimamia  udhibiti wa fedha kwenye shirikisho kwa kuziba mianya yote ya upotevu au matumizi ambayo hayana ulazima, kuongeza uwazi kwenye matumizi na mapato ya shirikisho pamoja na klabu.

Vilevile kutengeneza ushirikiano na wenzetu waliondelea katika Afrika na Duniani kwa ujumla  ili kuweza kuboresha  na kuendeleza ligi zetu. Nitapambana nakuongeza mapato kwa kutumia njia ya kisasa ya mawasiliano yaani Digital Platforms kwa kufanya streaming’ kwa kutumia siu za mikononi kwa kutumia Application yetu ambayo tutaitengeneza” ameeleza Mulamu.

Mambo mengine ni kuhakikisha kunaboreshwa Ligi zotekuanzia Ligi Kuu hadi Ligi ya Mabingwa wa mikoa kwa kuongeza udhamini.  Pia kuongeza timu shiriki za Ligi Kuu kutoka 16 hadi 20, ili kutanua wigo kwa wadhamini kujitangaza sehemu kubwa ya mikoa ya Tanzania.

Mgombea nafasi  ya Makamu wa Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF), Mulamu Erick Nghambi akizungumza na waandishi wa Habari mapema leo Agosti 7,2017, Jijini Dar es Salaam.

Bodi ya Ligi kuwa na mamlaka kamili kama kampuni isiyo na hisa chini ya shirikisho nchini hivyo kuzifanya  klabu kuendesha maamuzi yenyewe.” Alifafanua juu ya mipango yake hiyo ya muda mfupi bwana Mulamu.

Aidha kwa upande wa mipango ya muda mrefu, Bwana Mulamu ameweka wazi kuwa, atashirikiana na mikoa yote kuja na mpango mkakati wa kitaifa ambao utakuwa ndio dira ya mpira wa miguu nchini.

“Kufanya ukarabati kwa hosteli zetu  kwa kiwango cha kuwa nyota tatu. Hii itasaidia timu za Taifa ziweze kufikia hapo pindi zitakapohitaji kuingia kambini na itasaidia kupunguza gharama  ambazo zimekuwa zikitumika kulipia kambi katika hoteli mbalimbali na fedha hizo zitapelekwa kusaidia mpira katika maeneo mengine” amefafanua Mulamu.

Bwana Mulamu anaweka wazi kuwa, ili kuwa walipaji wazuri wa kodi hapa nchini, watahakikisha wanaweka mifumo ya mashine za kielektroniki kwenye viwanja vyote nchi nzima ili klabu kupata mapato halali na kupitia kupitia mfumo huo itasaidia Serikali kupata mapato yake.

Pia kuhakikisha kila mkoa unaendesha program ya kuendeleza Vijana  wenye umri chini ya miaka 13 (U-13) kupitia shule za msingi na Sekondari  kwa kushirikiana na TAMISEMI.

Mwisho ameahidi kuhakikisha anaboresha soka la Wanawake hii ni pamoja  na kupata timu bora za Ligi na ushindani.

“Kwa kushirikiana na Kamati ya  Utendaji na TFWA, tutahakikisha soka la Wanawake linaimarika kwa kuanzisha taratibu mahsusi za kupata Wasichana ili waweze kucheza soka kutoka  shule naa pia kupata walimu na waamuzi wa kike” alimalizia Mulamu katika mkutano wake huo wa ufunguzi.

Hadi sasa wagombea mbalimbali wapo katika kinyang’anyiro cha uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika hapo baadae ambapo kampeni zake zimeanza hii leo kwa wagombea hao kujinadi sera zao.

Na Andrew Chale,MO BLOG

Mgombea nafasi  ya Makamu wa Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF), Mulamu Erick Nghambi (katikati) akizungumza na wanahabari (Hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wake huo wa kampeni leo Agosti 7,2017, Jijini Dar e Salaam. Picha zote na Andrew Chale.

Share:

Leave a reply