Mzalishaji mbegu apata Tuzo ya Ujasiriamali ya Citi Foundation

91
0
Share:

Zabron Mbwaga ambaye ni Mzalishaji mbegu, aliyepo Viwanja vya NaneNane, Njiro mkoani Arusha ametwaa tuzo ya mshindi wa jumla wa tuzo za Ujasiriamali ya Citi Foundation. Tuzo hiyo inaambatana na fedha taslimu dola za Marekani 7,500.

Mbwaga ambaye aliwezeshwa upanuzi wa shughuli zake kwa mikopo kutoka BRAC Tanzania, alianza kazi zake akiwa na mtaji wa shilingi milioni 2 kabla ya kuongezewa nguvu na BRAC.

Tuzo hizo zilizofanyika mwishoni mwa wiki zilitolewa kwa wajasiriamali 16 na ofisa mikopo mmoja.

Mshindi wa pili ni Anney Sekulasa akiondoka na dola za Marekani 6000 huku mshindi wa tatu ni Lydia Majoro ambaye aliondoka na dola za Marekani 4000. Nafasi ya mjasiriamali mlemavu ilitwaliwa na Aneth Geraw aliyepata dola za Marekani 2000.

 Zaidi ya shilingi milioni 70 za kitanzania zimetolewa kwa washindi wa kwanza hadi wa 16 . Pia Taasisi za kifedha za wajasiriamali wadogo na wa kati (MFI) zenye ubunifu mkubwa wa bidhaa zake na huduma, mifumo ya kutolea huduma na methodolojia pia ilipata  tuzo. Safari hii Yetu Microfinance ndio walioinyakua.

Tuzo hizo za Citi Bank Foundation zimeendeshwa na Mtandao wa Asasi zinazotoa huduma za kifedha kwa wajasiriamali wadogo (TAMFI) ‘TAMFI’ na washindi wametangazwa na majaji walioshiriki kufanyakazi hiyo.

Tuzo hizo zimelenga kuhamasisha  wajasiriamali kutumia taasisi za kifedha za watu wa kati na chini na kufaidika nazo.

Takribani wajasiriamali 209 waliwasilisha miradi yao lakini 22 pekee ndio waliweza kupenya na 16 ndio walipata ushindi wa tuzo tofauti.

Safari hii washiriki walitoka maeneo mbalimbali nje ya Dar es Salaam tofauti na ilivyokuwa kwa mwaka 2016 ambapo washiriki wake walikuwa ni wa Dar es Salaam pekee.

Washindi wengine ni Comelord  Swai $ 1000, Prisca Kayombo $ 1000, Rahim Kalyango $ 1000, Emmanuel Lazaro $ 1000, Jumanne Findisha $ 1000, Salma Said $ 1000, Editha Lukindo $ 1000, Amon Kalumuna $ 1000, Salum Chumu $ 1000 na Doroth Sambi $ 1000.

Share:

Leave a reply