Ngoma ya Kiumbizi kutoka Pemba yapamba tamasha la Sauti za Busara 2017

1212
0
Share:

Tamasha la Sauti za Busara msimu wa 14 limefika tamati usiku 12 Februari 2017, huku vikundi mbalimbali vikiweza kukonga nyoyo za wadau wa burudani waliojumuika kutoka sehmu tofauti Duniani ambao kwa pamoja walikusanyika kwenye viunga vya Ngome Kongwe  mjini Unguja, Zanzibar.

Mchana wa 12 Februari, kikundi cha Ukakamavu maarufu  kama ‘Kiumbizi’ kutoka  visiwani Pemba, kiliweza kuonesha vyema ukakamavu wao katika kucheza ngoma hiyo ya Kiumbizi.

MO Blog,  ilipata kufanya mahojiano na kundi hilo la Kiumbizi ambapo kwanza waliweza kutoa ufafanuzi wa asili ya ngoma hiyo na aina ya uchezaji ni asili ya watu wa kutokea Pemba ambao waliamua kuanzisha mchezo huo wa kuzunguka na kisha kupigana na fimbo ndio maana ya ‘Kiumbizi’  ili kujihami kutoka mateso ya Wakoloni wa Kireno ambao waliwatesa kwa kuwachapa mara kwa mara na fimbo  hizo ambazo zilikuwa zikiwajeruhi na hata kuwasababishia vifo.

“Wazee wetu baada ya kuchoka kupigwa na fimbo kutoka kwa wakoloni wa Kireno. Waliitana nje ya kaya zao yaani kwenda porini na kisha wakapanga mipango ya asili ambayo ilikuwa ni kuchukua hatua pindi wanapochapwa na fimbo.  Kweli mipango yao ilifanikiwa lakini baada ya kushtukiwa ikabidi wabadilishe mchezo huo na kisha kuutumia kama ngoma ya asili ili wareno wasijuie, hivyo hali hiyo iliendelea na mpaka leo sie tumeamua kuenzi” alieleza Katibu wa Kiumbizi Juma Omary  Seif ambaye pia ameeleza kuwa kikundi hicho kilianzishwa rasmo tokea mwaka 1998.

Naye Afisa Utamaduni wa Wilaya ya Chake, Bi. Awali Musa Msafiri ambaye pia ni mmoja wa viongozi wa kikundi hicho ameeleza kuwa, wameamua kuenzi mchezo huo  kwani unasaidia pia ukakamavu kwa wananchi pamoja na kuenzi tamaduni za awali za mababu..

Mpaka sasa kikundi hicho cha Kiumbizi  ni mara ya pili kushiriki tamasha hilo kubwa la Sauti za Busara ambapo wameeleza kufurahia kwa watu kuwapokea na kufurahia michezo yao hiyo hasa ule wa kipiganana fimbo.

Fimbo zinazotumika ni za kweli na mchezo unaochezwa pale wa kuchapana watu wote wamekuwa kwenye mazoezi na wanatakiwa kuwa makini namna ya kuidaka fimbo hiyo pindi wanapopigana ama namna ya kuvumilia ili isimzuru zaidi, ila kuna wakati wanaumia vilivyo.

Kiuzoefu tayari kundi hilo la Kiumbizi limeweza kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kiserikali na kivyama ambapo wao wakichezao michezo yao hiyo na aina mbalimbali za ngoma za asili.

Tamasha la mwaka huu la Sauti za Busara 2017, limeweza kukusanya vikundi 40, wenye jumla ya wasanii 400 ambao kwa pamoja wameweza kutumbuiza kwenye majukwaa matatu tofauti, kuanzia 9-12 Februari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Busara Promotions ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara, Yusuf Mahmoud ‘DJ Yusuf’ akibadilishana mawazo na wageni mbalimbali waliofika kuangalia tamasha hilo la Sauti za Busara 2017. Pichani ni katika jukwaa la Busara la Forodhan.

Mwendeshaji wa shughuli MC katika majukkwaa ya Forodhan na lile la Amphiether ndani ya Ngome Kongwe, Muslim Nassor ‘Jazzphaa’ akifungua jukwaa hilo muda mfupi kabla ya kuanza kwa maonesho ya vikundi vya Ngoma

Kiongozi wa kundi la Kiumbizi,  Juma Omary  Seif akiongoza kundi hilo kwenye onesho lao hilo la Sauti za Busara 2017

Ngoma hiyo ya Kiumbizi ikichezwa jukwaani kwenye tamasha la Sauti za Busara 2017. Picha zote na Andrew Chale-MO BLOG-Zanzibar.

Share:

Leave a reply