modewji

 

Mohammed Dewji alizaliwa tarehe 8/05/1975 , mjini Singida kata ya Ipembe. Ni kwa majaliwa ya Mwenyezi Mungu Mo alizaliwa salama, kwani mama yake mzazi alijifungua akiwa nyumbani lakini alisaidiwa na nesi na daktari. Ni mtoto wa pili wa Mzee Gulam Dewji katika watoto sita wa familia hiyo. Ana dada mmoja Sabera na wadogo zake Ali, Hassan, Hussein na Fatema.Baada ya kufikisha umri wa miaka mitano, alihama na kwenda mkoa wa Arusha kwa ajili ya elimu ya shule ya msingi. Aliishi Arusha na kusoma katika Shule ya msingi ya Arusha hadi mwaka 1986 alipohitimu elimu ya msingi.

Mwaka 1987 alihamia Dar es Salaam kwa ajili ya masomo ya sekondari na alijiunga na shule ya kimataifa ya Tanganyika (IST), hapo Mo alimaliza elimu yake ya Sekondari mwaka 1992. Na huu ndio ukawa mwisho wake wa kusoma nchini Tanzania .

Mwaka 1992 alienda kuongeza elimu mara hii akisafiri kwenda nje ya nchi kutafuta elimu na kufanikiwa kuingia katika Shule ya SaddleBrooke High School ya Marekani. Akiwa hapo ndipo Mo alipoanza kuonyesha dalili za kwanza za kuwa na sifa za uongozi pale aliposhika nafasi ya kuwa Rais wa wanafunzi wa shule ya SaddleBrooke. Kushika nafasi kama hiyo katika nchi ngeni lilikuwa ni jambo la kujivunia na heshima kubwa kwa familia na pia Watanzania kwa ujumla. Pamoja na kuwa na nafasi ya uongozi akiwa shuleni Marekani, Mo alipigiwa kura hapo shuleni ya kuwa kati ya wanafunzi waliofanya vizuri au tunaweza tukasema wenye vipaji( Most Accomplished student) na upande wa wanawake aliyepigiwa kura hapo mwaka huu alikuwa ni mchezaji maarufu wa tenisi duniani wakati ule Jeniffer Capriati.

Alipomaliza elimu yake hapo Saddle Brooke , Mo alipata nafasi ya kujiunga na moja kati ya vyuo vikuu bora duniani, GeorgeTown University iliyokuwa jijini Washington D.C, Marekani. Alisomea mambo ya biashara ya kimataifa na fedha, huku akichukua Theolojia kama somo la ziada.

Katika kipindi hicho cha masomo katika chuo cha GeorgeTown ndipo Mo alipoanza kubadilika kimaisha na kubadili mtazamo mzima wa kuangalia mambo ambayo binadamu anayafanya kila siku. Chuo hicho kinasifika kuwa na elimu bora na kimetoa viongozi na watu ambao wamefanikiwa sana katika maisha mfano Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton, Mfalme Abdullah wa Jordan, Rais Gloria Arroyo wa ufilipino na hata wachezaji wa mpira wa kikapu maarufu nchini Marekani kama Allen Iverson na Patrick Ewing.

Alipohitimu masomo mwaka 1998 alirudi nyumbani Tanzania na moja kwa moja akaingia kwenye biashara za baba yake Mzee Gulam na akaanza na nafasi ya Mdhibiti mkuu wa Fedha katika kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (METL).

Mbali na kuingia kwenye biashara, Mo alijiingiza kwenye michezo na kuanza kuifadhili Simba Sports Club ya Dar es Salaam. Huu ukawa mwanzo wa Watanzania kumuona Mo akiingia kwenye ulimwengu wa michezo wa Tanzania na hasa soka.

Ilipofika mwaka 2000, uchaguzi wa pili wa mfumo wa vyama vingi nchini uliwadia. Na Mo akajiingiza kwenye kinyanganyiro hicho akiwania kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM katika jimbo la Singida mjini. Katika kura za maoni Mo alimshinda Waziri wa Maji wa wakati huo Musa Nkhangaa kwa kura nyingi lakini kamati kuu ya CCM hawakumpitisha kugombea ubunge.

Kuna usemi mvumilivu hula mbivu, hivyo Mo akakubali na kuheshimu maamuzi ya chama na kumpigia kampeni mgombea wa chama na kuhakikisha wanashinda Uchaguzi wa 2000.

Pamoja na kushindwa kupata nafasi ya kugombea ubunge, Mo aliwasaidia wananchi wa Singida kwa hali na mali , huku pia akizidi kutoa mikataba minono ya udhamini kwa Simba iliyokuwa inazidi Milioni mia moja kwa mwaka.

Mwaka 2001 Mo aliamua kuachana na ukapera na kuamua kumuoa Saira, ambaye walijuana tokea enzi za shule. Kila kitu kinapangwa na Mungu kwani Mo alienda kusoma Marekani na kupoteza mawasiliano na Saira, lakini aliporudi kutoka Marekani ndipo wanandoa hao walianza kujuana zaidi na hatimaye kuamua kufunga ndoa ambapo wamejaliwa kuwa na watoto wawili, mmoja wa kike aitwaye Naila mwenye umri wa miaka sita na wa kiume anaitwa Abbas mwenye umri wa miaka mitatu.

Miaka miwili baada ya ndoa Mo alipanda cheo katika kampuni ya familia na kukabidhiwa rasmi kampuni nzima kama Mkurugenzi mkuu wa Mohammed Enterprises Limited (METL). Chini ya uongozi wake kampuni imepanda ngazi nyingi za mafanikio na kukua mara nane ya kiwango alichokikuta kuanzia pale alipoanza kufanya kazi, amewekeza kwenye sekta tofauti kama Kilimo, Fedha, Uzalishaji na Usambazaji wa bidhaa.

Takwimu zinaonyesha kampuni za Mo zinachangia pato la ndani la taifa kwa asilimia mbili na zinaajiri zaidi ya watu 20,000.

Mwaka 2005 ulikuwa mwaka wa uchaguzi na MO akachukua fomu tena za kuwania ubunge wa jimbo la Singida mjini. Kwa mara nyingine aliibuka kidedea katika kura za maoni akipitishwa na kamati kuu ya CCM kuwa mgombea na baada ya hapo akawabwaga wapinzani wake katika uchaguzi kwa kuchaguliwa kwa zaidi ya asilimia tisini ya kura zote zilizopigwa.

Tarehe 29 /12/2005 Mohammed Dewji ‘Mo’ aliapishwa kuwa Mbunge wa Singida mjini, na kuwa mwakilishi rasmi wa kero za wananchi wa Singida mjini bungeni.

Michezo na Mo hawakai mbali mbali. Rais Kikwete alikuja na ari mpya na kuwafanya Watanzania kupenda michezo na hasa timu yao ya taifa ya soka, Taifa Stars. Ili kufanikisha na kuleta maendeleo ya Stars kamati maalumu ya ushindi iliundwa huku Mo akiteuliwa kuwa Mwenyekiti wake. Katika kipindi chake Taifa Stars wamebadilika kutoka kuwa kichwa cha mwendawazimu na kuwa timu inayoheshimika barani Afrika ikitoa sare na vigogo wa soka kama Cameroon na Senegal .

Pia chini ya uenyekiti wake Taifa Stars imepata kushiriki michuano mikubwa barani Afrika ya CHAN yaliyofanyika nchini Ivory Coast .

Mwaka 2007 kulikuwa na uchaguzi wa viongozi wa Chama (CCM) na Mo alijitosa na kuwania kugombea nafasi ya mjumbe wa Halmashauri ya taifa (NEC) na akafanikiwa kushinda kwa kupata kura za kutosha na kuweza kufanikisha azma yake hiyo.

Hii ni historia fupi ya Mhe. Mohammed Dewji ( Mbunge, Mjumbe wa Halmashauri ya Taifa (NEC) na mkurugenzi wa makampuni ya Mohammed Enterprises) ambaye anaendelea kusaidia jimbo na taifa lake kwa hali na mali pale anapokuwa na uwezo na nafasi ya kufanya hivyo.

le ya kimataifa ya Tanganyika (IST), hapo Mo alimaliza elimu yake ya Sekondari mwaka 1992. Na huu ndio ukawa mwisho wake wa kusoma nchini Tanzania .