NMB Bank yakabidhi vifaa vya michezo kwa timu ya Bunge

845
0
Share:

Kuelekea bonanza la michezo ya kirafiki kati ya timu ya Benki ya NMB dhidi ya timu ya Bunge kwa mchezo wa mpira wa miguu, mpira wa kikapu na mpira wa mikono, benki ya NMB imekabidhi vifaa vya michezo kwa timu ya Bunge vilivyo na thamani ya milioni saba.

Akizungumza kuhusu vifaa hivyo, Meneja wa Wateja Wadogo na Kati wa NMB, Abdulmajid Nsekela alisema wamekabidhi vifaa vya soka, mpira wa pete na kikapu kwa ajili ya kutumika katika bonanza la michezo ambapo timu ya NMB na Bunge zitakuwa zikishindana, bonanza ambalo litafanyika leo jumamosi katika Uwanja wa Jamhuri.

“Wabunge tunafahamu wanahusika katika ujenzi wa nchi lakini wakiwa na afya bora hata sheria watatunga nzuri zaidi, sisi kama NMB ili mechi ipendeze lazima wabunge wetu wang’ae,

“Imani yetu ni michezo hii itatumika kama kielelezo cha mshikamano wetu ili tuweze kuboresha afya zetu na kuboresha uhusiano,” alisema Nsekela.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bunge Sports Club, William Ngeleja alisema timu zao zimekuwa zikikutana mara kadhaa na michezo itakayopigwa leo ni sehemu ya mwendelezo wa ushirikiano wa Bunge na benki ya NMB.

“Katika mara zote ambazo tumekutana hawajawahi kutufunga, wakijitahidi sana ni kutoa sare, kikubwa katika michezo hii ni kuimarisha uhusiano, bunge kama chombo cha kuwakilisha wananchi kinaendelea kuimarisha uhusiano na taasisi zingine ambazo zinashiriki kuendeleza uchumi na maendeleo ya taifa letu,” alisema Ngeleja.

Share:

Leave a reply