NMB yaahidi kuboresha huduma za kijamii Zanzibar

486
0
Share:

Benki ya NMB Tanzania imeiahidi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa itaendelea kusaidia wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba kwa kuboresha huduma za kijamii ili kuwezesha wananchi kuwa na maisha bora.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Bi. Ineke Bussemaker wakati alipofanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Serikali ya Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ambapo walizungumzia mambo mbalimbali yanayohusu utendaji kazi wa NMB na mipango waliyonayo visiwani humo.

Mkurugenzi huyo aliahidi kuwa NMB itaendelea kusaidia miradi mbalimbali katika jamii kama ya elimu, kilimo, afya ikiwa na lengo la kuwaunga mkono wananchi katika kujiletea maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii ili waweze kuondokana na janga la umasikini.

Aidha Bi. Bussemaker alipongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Shein katika kuimarisha miradi ya maendeleo katika jamii kwani hilo ndilo hitaji la wananchi na wao kama NMB wataendelea kushirikiana.

Kwa upande wa Rais Shein, aliishukuru benki ya NMB kwa mchango ambao imekuwa ikiutoa kwa wananchi wa Zanzibar lakini pia kutumia fursa hiyo kumueleza Mkurugenzi Mkuu huyo wa NMB juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kupambana na changamoto ya ajira kwa vijana ikiwa ni pamoja na lengo la Serikali la kuanzisha uvuvi wa bahari kuu.

Share:

Leave a reply