Pizza Hut yazindua kampeni ya kuhamisha watoto kusoma

72
0
Share:

Kampuni ya Pizza Hut Africa imezindua kampeni ya Slice of Africa (Kipande cha Afrika) kwa hapa nchini ambayo inahamasisha watoto kusoma na inatarajiwa kufanyika katika miji 14 ya nchi 12 zilizopo Afrika.

Akizungumza kuhusu kampeni hiyo, Meneja Mkuu wa Pizza Hut Afrika Ewan Davenport alisema ilianzishwa rasmi mwaka 2016 ili kuhamasisha elimu kupitia utoaji wa rasilimali na kushirikisha wateja ili kuleta mabadiliko katika jamii.

Alisema katika mwaka wake wa kwanza kampeni hiyo ilinufaisha zaidi ya watu milioni 15.9 na ilisambaza zaidi ya vitabu 275,000 na vifaa vingine vya elimu katika jamii za Marekani kaskazini ikiwemo Canada, Costa Rica na Afrika Kusini.

“Badala ya kusambaza pizza tunasambaza viboksi vya rangi nyekundu (Red Reading Boxes) tukishirikiana na shirika lisilo la kiserikali ‘READ Educational Trust’, katika kutafuta njia za kivumbuzi za kuendeleza elimu kwa ajili ya watoto katika kila nchi,” alisema Davenport na kuongeza.

“Kutokana tafiti zinazosema kwamba zaidi ya watoto milioni 280 barani Afrika hawajui kusoma, kampeni hii ni muhimu sana. Elimu na kujisomea ni fursa kubwa katika kuleta maendeleo na tumelenga kutumia ukuaji wa migahawa yetu barani Afrika ili kuleta mabadiliko katika jamii tunazotumikia.”

Katika safari yao timu hiyo ya ‘Slice of Africa’ ikiwa na wafanya biashara wa kampuni hiyo ya Pizza Hut watazindua kampeni ya kujitolea kwa wateja katika kila nchi ili kukusanya fedha zitakazojumuishwa na za kampuni hiyo ili kuweza kusambaza maboksi mengi zaidi.

Katika kila nchi Pizza Hut imechagua shirika lisilo la kiserikali ambalo litafanya kazi ya kutambua walengwa kutoka katika mashirika au shule watakaopatiwa boksi hizo nyekundu. Watoto kutoka shirika la Room to Read wameambatana na timu ya Davenport nchini katika kampeni hii.

Share:

Leave a reply