Polepole azungumza kuhusu Nyalandu kujivua uanachama, asema ni afya kwa demokrasia

365
0
Share:

Katibu wa itikadi na Uenezi wa CCM , Humphrey Polepole amesema uamuzi uliochukuliwa na Mbunge wa Singida Kaskazini kwa tiketi ya CCM, Lazaro Nyalandu wa kujivua uanachama wa chama hicho na ubunge ni jambo la kawaida.

Polepole aliyasema hayo alipokuwa akifanya mahojiano na kituo cha runinga cha ITV na kusema CCM inatambua haki za msingi za kila raia na uamuzi wa Nyalandu kujivua uanachama kwao walipokea kama habari ya kawaida lakini pia ni afya kwa demokrasia ya nchi.

“Sisi kama chama kilichopo madarakani tunatambua haki za Mtanzania zikiwepo za kiasiasa kwa hiyo mtu yoyote ambaye anaondoka katika Chama cha Mapinduzi ni jambo la kawaida sana, kwetu sisi ni habari za kawaida kabisa,

“Katika historia wamepata kuondoka watu ambao wameitwa vizito, vigogo kwenye Chama cha Mapinduzi na huyu aliyeondoka ni mwanachama wa kawaida wa Chama cha Mapinduzi kwahiyo ni jambo la kawaida na ni afya kwa demokrasia,” alisema Polepole.

Nyalandu alitangaza uamuzi wa kujivua uanachama wa CCM na ubunge jumatatu ya Oktoba, 30 na kuomba wanachama cha Chadema kumpa nafasi ya kujiunga na chama hicho, ombi ambalo lilijibiwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na kumwambia kuwa milango ipo wazi.

Share:

Leave a reply