Polisi Dar yawatia mbaroni watu 267

1682
0
Share:

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekamata watuhumiwa 267 kwa makosa mbalimbali ikiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha, utapeli, wizi, kucheza kamari, na kupatikana kwa dawa za kulevya, kuanzia Aprili 13 hadi 17,2017.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 19, 2017 Jijini Dar es Salaam, Kamishna wa kanda hiyo, Kamanda Simon Sirro amesema takribani kete 366 za dawa za kulevya, bhangi misokoto 51 na lita 200 za pombe haramu aina ya gongo zilikamatwa kufuatia operesheni kali iliyofanywa na askari polisi.

“Pia Polisi wamekamata watuhumiwa watatu kwa wizi wa vitu mbalimbali maeneo ya Chamanzi wanaofahamika kwa majina ya Athuman Bashiru na Rashid Seleman na Mohamed Mussa. Pia wamekamata pikipiki moja ya wizi na kwamba watuhumiwa wawili wanashikiliwa kufuatia tukio hilo ambapo walimkata na panga kichwani mmiliki wake Ibrahim Shaban na kumpora pikipiki hiyo,” amesema.

Aidha, amesema Jeshi la Polisi mnamo Aprili 10, 2017 limekamata watuhumiwa watano wa ujambazi ambao hushirikiana kufanya matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali ya jiji.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Salimu Matanda, Eliaki Chaki, Shaban, Rashid Said, na Nassoro Choro ambao wamekamatwa baada ya kuiba pikipiki aina ya Boxer inayomilikiwa na Noel Mkinga.

Katika tukio lingine, Kamanda Sirro amesema Jeshi la Polisi lilikamata silaha moja aina ya Shotgun maeneo ya Kiwalani iliyofutwa namba za usajiri baada ya wahalifu waliokuwa nayo kuitekeleza walipokuwa wanakimbizwa na Polisi.

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply