Polisi Tabora wakamata watu wengine 37 wakihusishwa kuchoma moto wanawake wanne

629
0
Share:

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linawashikiria watu 44 wa kijiji cha Mwamabondo wilayani Uyui kwa tuhuma za kuwashambulia silaha za jadi na kuwauunguza kwa moto wanawake waanne wakiwatuhumu kuwa wachawi na wanahusika na kifo cha mume wa mmoja wao.

Kauli hiyo imetolewa jana mjini hapa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora Wilboard Mtafungwa wakati wa mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake.

Alisema kuwa idadi hiyo inafuatia 37 kukamatwa na kuunganishwa na wale saba ambao walikamatwa hapo awali kufuatia tukio hilo na kufikisha 44.

Kamanda Mtafungwa alisema kuwa wanawake hao walitendewa unyama huo na wanakijiji hicho baada ya kuwakamata na kuwahoji kuhusiana na thuma za kufanya vitendo vya kishirikina hapo kijijini.

Alisema baada ya kuwahoji wanakijiji walipitisha azimio kuwa wakinama hao wauwawe kwa kuchoma moto na ndipo walipofungwa vitambaa usoni wakiwa uchi na kusambuliwa na fimbo sehemu mbalimbali za miili yao kisha wakaanza kukusanya kuni na nyasi kwa lengo kuwachoma ili wateketee kabisa.

Kamanda Mtafungwa alisema kuwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema wanaochukizwa na vitendo hivyo vya kikatili, waliamua kutumia  askari wakiwa doria katika eneo la vijijini ili kuokoa maisha ya wanawake hao.

Alisema kuwa chanzo cha tukio zima ni kifo cha Mafumba Tilawisi ambaye alikuwa mume wa mmoja wa wanawake walioshambuliwa Manugu Lutema .

Kamanda Mtafungwa alisema kuwa baada ya kifo chake taarifa zilisambaa na watu wakakusanyika kwa ajili ya maandalizi ya mazishi na ndipo zilianza kujitokeza tuhuma kuwa marehemu aliwawa kwa njia za kishirikina na mke wake Manugu Lutema.

Alisema kuwa ndipo watu wenye hasira waliamua kumukamata na kutaka ataje wenzake anaoshirikiana nao katika vitendo vya kishirikina na ndipo aliwataja wengine kwa hofu kuwawa ambao ni Elizebeth Kashindye, Maria Sahani, Manugwa Lutema na Rahaeli Mikomangwa.

Kamanda Mtafungwa alisema kuwa msako huo utaendelea hadi wale waliohusika na tukio hilo wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya Sheria.

Na Tiganya Vincent, Tabora

Share:

Leave a reply