Rais Magufuli Aagiza TCU kutowachagulia Wanafunzi wa Elimu ya Juu Vyuo

904
0
Share:
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU)
kutowachagulia vyuo wanafunzi wa elimu ya juu na kuwaacha wanafunzi hao
kuchagua vyuo wanavyovitaka wenyewe.
Agizo hilo limetolewa leo, Jijini Dar es
Salaam Rais Magufuli alipokuwa akizindua Mabweni mapya ya Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam ikiwa ni ahadi yake aliyoitoa Chuoni hapo Juni, mwaka jana.
“Ninaamini kama wanafunzi wangepewa nafasi
ya kuchagua vyuo wanavyovipenda wenyewe, vyuo vya Serikali kama vile Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) Chuo Kikuu cha
Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu cha Mzumbe vingekuwa na wanafunzi wengi sana,”
alisema Dkt. Magufuli.
Aliendelea kwa kusema kuwa TCU imekuwa
ikiwachagulia wanafunzi vyuo visivyo na sifa na makazi ya wanafunzi hivyo
kusababisha wanafunzi hao kusoma katika mazingira magumu na wanapomaliza masomo
yao hukosa ajira kutokana na vyuo hivyo kutokuwa na sifa.
Aidha, Rais Magufuli ameuagiza uongozi wa
UDSM kutoza wanafunzi gharama ya shilingi mia tano(500) kama malipo ya makazi
ya  mabweni hayo kwa siku badala ya
shilingi mia nane(800) inayotozwa kwa mabweni mengine yaliyopo chuoni hapo.
Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
imejipanga kuwekeza katika elimu hivyo itahakikisha wanafunzi nchini
wananufaika kwa kupata elimu bora kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu.
“watanzania walinichagua ili kutatua
changamoto zinazowakabili na hivi ndivyo ninavyofanya kutatua changamoto hizo”
alisema Rais Magufuli.
Naye, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia
Prof. Joyce Ndalichako amempongeza Rais Magufuli kwa kutoa shilingi bilioni 10
kwa ajili ya ujenzi wa mabweni hayo ambao kwa kiasi kikubwa yatatatua
changamoto ya makazi iliyokuwa ikiwakabili wanafunzi wa chuo hicho.
Prof. Ndalichako amesema kuwa mabweni hayo
yamejengwa kwa kipindi cha miezi 8 ambayo yatachukua wanafunzi 3840.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha
Kikuu cha Dar es Salaam Prof. Rwekaza Mukandala ametoa rai kwa wanafunzi wa
chuo hicho kuhakikisha wanaimarisha usalama katika maeneo ya mabweni hayo na
kulinda miundo mbinu yote iliyoweka.
“Ni lazima mzingatie matumizi sahihi ya
kila kifaa kilichofungwa katika majengo haya, majengo haya ni mapya na
yamejengwa kwa gharama kubwa kwa lengo la kutusaidia kuondokana na changamato
iliyotukabili kwa muda mrefu,” alisema Prof. Mukangala.
Wakati huohuo Rais Magufuli ameweka jiwe la
msingi mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi magomeni “QUARTERS”, mradi ambao kwa
asilimia kubwa unawagusa watanzania wa hali ya chini.
Aidha Rais Magufuli ameendelea kusisitiza
juu ya ahadi aliyoitoa kwa wakazi 644 waliokuwa wakiishi maeneo hayo kupewa
nyumba ambapo wataishi bure kwa muda wa miaka mitano.
Pia, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo
(TBA) Msanifu Majengo Elvis Mwakalinga amesema ujenzi wa mradi huo umezingatia
miundombinu yote iliyohitajika ambapo itakuwa na sehemu za makazi, biashara,
maegesho ya magari na bustani ya kupumzikia.
Ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kutekelezwa
katika kipindi cha mwaka mmoja ambapo ujenzi wake ulianza rasmi Octoba mwaka
jana.

Na Lilian Lundo na Beatrice Lyimo
Share:

Leave a reply