Rais Magufuli akutana na Mjumbe wa Kamati kuu ya CPC ya China Ikulu Dar

627
0
Share:

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 22 Machi, 2017 amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Katibu wa Kamati ya CPC ya Manispaa ya Beijing nchini China Mhe. Guo Jinlong.

Katika Mazungumzo hayo Mhe. Guo Jinlong amewasilisha salamu za Rais wa China na Katibu Mkuu wa CPC Mhe. Xi Jinping ambaye amempongeza Mhe. Dkt. Magufuli kwa juhudi zake za kuimarisha uchumi wa Tanzania, kupambana na rushwa na kufanya mageuzi yenye lengo la kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa manufaa ya Watanzania.

Mhe. Guo Jinlong amesema uhusiano na ushirikiano mzuri kati ya China na Tanzania ulioasisiwa na Mwenyekiti Hayati Mao Tse-tung na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere utaendelezwa na kuimarishwa zaidi na kwa namna ya kipekee ameishukuru Tanzania kwa kuiunga mkono China katika masuala ya kimataifa.

Aidha, Mhe. Guo Jinlong ameahidi kuwasilisha katika Kamati Kuu ya CPC ombi la Tanzania kuikaribisha China kushirikiana katika ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kwa kipande cha kuanzia Morogoro hadi Dodoma na pia ombi la kulikaribisha Shirika la Ndege la China kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Beijing na Dar es Salaam ili kukuza utalii, uwekezaji na biashara.

“Nimefurahi sana kwa kutupokea vizuri na ninakuhakikishia kuwa tutaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya uhusiano wetu ikiwemo kuendeleza kilimo na viwanda nchini Tanzania” amesema Mhe. Guo Jinlong.

Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Guo Jinlong kwa kuja nchini Tanzania na kumletea ujumbe wa Mhe. Rais Xi Jinping.

Mhe. Dkt. Magufuli amesema Tanzania itaendelea kuuthamini na kuukuza uhusiano na ushirikiano wake na China na amemuomba Mhe. Guo Jinlong kuwashawishi wawekezaji na wafanyabiashara wa China kuja Tanzania kuwekeza katika sekta mbalimbali hususani viwanda, ujenzi wa miundombinu ya usafiri na majengo na kuendeleza kilimo.

“Naomba unipelekee ujumbe kwa Mhe. Rais Xi Jinping kuwa namkaribisha sana Tanzania na namhakikishia kuwa Tanzania ipo tayari wakati wowote kushirikiana na China katika maendeleo na mambo mengi yenye manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia utiaji saini wa mikataba mitatu ya misaada iliyotolewa na Serikali ya China kwa Tanzania ambayo ni msaada wa upanuzi wa Shule ya Polisi Tanzania iliyopo Moshi Mkoani Kilimanjaro, msaada wa Dola za Marekani 300,000 kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na msaada Dola 20,000 kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za Serikali kupambana na dawa za kulevya.

Na Gerson Msigwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU Dar es Salaam

Share:

Leave a reply