Rais Magufuli amteua Prof. Frolens Luoga kuwa Gavana wa BOT

265
0
Share:

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemteua Prof. Frolens Dominic Andrew Makinyika Luoga kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Prof. Luoga anachukua nafasi ya Prof. Benno Ndulu ambaye anamaliza muda wake.

Prof. Luoga ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taaluma).

Mhe. Rais Magufuli ametangaza uteuzi huu leo tarehe 23 Oktoba, 2017 katika hafla ya kuwatunuku vyeti vya shukurani na pongezi wajumbe wa kamati zilizofanya uchunguzi wa aina, kiwango na thamani ya madini yaliyokuwemo katika makinikia, iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo Mhe. Rais Magufuli amewatunuku vyeti wajumbe wote 28 wa kamati hizo kwa kutambua mchango mkubwa wa kila mmoja wao katika uchunguzi na majadiliano kuhusu rasilimali za madini na matokeo ya kazi yao ambayo yameiletea nchi na Serikali faida na heshima kubwa.

“Uzalendo wako, jitihada zako binafsi na ushirikiano wako kwa wajumbe wa kamati katika kupigania  maslahi makubwa ya nchi yetu ni jambo la kupigiwa mfano na litakaloenziwa daima.

“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wananchi wa Tanzania na mimi binafsi, nakushukuru na kukupongeza sana” imenukuliwa sehemu ya shukurani na pongezi hizo za Rais Magufuli.

Miongoni mwa waliotunukiwa cheti cha shukurani na pongezi ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai kwa kutambua uzalendo wake, jitihada zake binafsi na ushirikiano wake mkubwa kwa Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kupigania maslahi makubwa nchi, jambo ambalo ni la kupigiwa mfano na litakaloenziwa daima.

Mhe. Rais Magufuli amewashukuru Watanzania wote kwa kuunga mkono jitihada za kupigania rasilimali za nchi na amewataka wawapuuze wanaobeza jitihada hizo pamoja na kuzitaka mamlaka husika kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanaotoa takwimu za upotoshaji kwa lengo la kuwagombanisha wananchi na Serikali.

Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara na wawekezaji na ametoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara kwa kuwa Serikali inawapenda na itaendelea kuwaunga mkono.

Katika hafla hiyo, viongozi mbalimbali wakiwemo wa dini, vyama vya siasa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Mhe. Mussa Azzan Zungu wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa jitihada kubwa alizozifanya katika kupigania maslahi ya Watanzania katika biashara ya madini na wameahidi kuendelea kumuunga mkono na kumuombea.

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

23 Oktoba, 2017

Share:

Leave a reply