Rais Magufuli atoa maagizo mazito kwa ATCL

220
0
Share:

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli ametoa maagizo kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Bodi ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kuwafukuza kazi pamoja na kuwachukulia hatua wafanyakazi wa shirika hilo watakao kiuka mikataba yao na kuisababishia hasara.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua ndege mbili mpya za serikali na kutia saini mkataba wa ukodishaji ndege baina ya serikali na ATCL.

Dk. Magufuli amesema serikali itaikodisha ndege hizo ATCL ambapo itailipa serikali sehemu ya mapato yake, ili iache kuitegemea serikali katika uendeshaji wake pamoja na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

“Tutawakodisha ndege ATCL ili waache kufanya kazi kwa mazoea, ninaitaka kufungua akaunti maalumu ya fedha benki ili kuweka mapato yatakayopatikana pindi ndege hizo zitakapoanza kufanya kazi, na kama mapato yatakuwa mazuri tutaiachia ndege hizo na kisha serikali kununua ndege nyengine, ” amesema.

Ameitaka ATCL kudhibiti mianya ya rushwa, ukwepaji kodi na ufujaji wa mali za shirika hilo ili lisijiendeshe kwa hasara.

“ATCL mkajipange vizuri katika upangaji wa ruti, bodi msiruhusu mtu kusafiri bure, hata mimi nikija mnitoze nauli, hata Waziri Mbarawa akija atozwe nauli, hivyo ndivyo biashara inakwenda, mwisho wa siku mtapimwa kwa utendaji kazi wenu, mtakapo haribu kazi hao viongozi hawatakuja kuwatetea, ” amesema.

Ametoa onyo kwa wafanyakazi wasio na uwezo wa kufanya kazi katika shirika hilo kuacha kazi kabla hawajatumbuliwa na kwamba serikali iko tayari kulipa fidia zao pindi watakapofanya hivyo.

“Wale waliojipanga kwenda na mwendo huu tutakwenda nao, wanaohisi hawezi kwenda na kasi hii waachie ngazi tutawapa malipo yao, “

Aidha ameitaka bodi ya ATCL kutoa huduma nzuri na kuzingatia ratiba ili kushindana katika soko la usafiri wa anga.

“Ndege mmezipata, mkizitumia vibaya hazitatufikisha popote. Mnaingia kwenye ushindani wa kweli. Ukitaka kukuza uchumi na sekta ya utalii lazima uwe na ndege inayofanya kazi vizuri, ” amesema.

Amesema ndege hizo zitasaidia wananchi wa vipato vya chini kwa kuwa zinauwezo wa kutua kiwanja chochote.

“Ndege hii inatua popote wananchi wa Dodoma, Songea, Mtwara, Musoma, Kigoma, Mafia na Zanzibar watanufaika na usafiri huu, ” amesema.

Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Emmanuel Korosso ameishukuru serikali kwa kulifufua shirika hilo na kuadi kuzitunza ndege hizo mpya ili zidumu kwa muda mrefu pamoja na kuiletea faida serikali.

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply