Rais Magufuli aweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya juu Ubungo

857
0
Share:

Rais John Pombe Magufuli leo Machi 20, 2017 ameweka jiwe la masingi la ujenzi wa barabara za juu (Interchange) katika makutano ya Ubungo utakaochukua miezi 30 kuanzia sasa hadi mwezi Septemba 2019, mradi mbao utagharimu takribani shilingi bilioni 188.71 ukiwa na lengo la kupunguza msongamano wa magari katika barabara za Morogoro, Nelson Mandera na Sam Nujoma.

Fedha za mradi wa ujenzi wa barabara zenye ghorofa tatu, umefadhiliwa na Benki ya Dunia ambayo imetoa zaidi ya bilioni 186.7 kwa ajili ya gharama za usanifu, usimamizi na ujenzi wa mradi wakati serikali ikichangia zaidi ya bilioni 1 kwa ajili huduma nyingine ikiwemo ulipaji fidia wa nyumba zitakazoathiriwa na mradi huo. 

Wakati akihutubia wananchi na wageni waalikwa waliohudhuria katika sherehe za uwekaji jiwe la msingi, Dkt. Magufuli ameitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi  kupitia  Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kumsimamia mkandarasi kampuni ya China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC)kujenga barabara za viwango pamoja na kukamilisha ujenzi wake haraka.

“Fedha hizi tutazisimamia kikamilifu, hakuna atakaye zichota fedha na atakayezitumia atatumbuliwa. Wizara ya ujenzi na kandarasi iliyopewa dhamana ya ujenzi ifanye kazi usiku na mchana ili miezi ipungue badala ya miezi 30 iwe miezi 20 sababu watanzania wanasubiri kuzitumia barabara hizi,” amesema Dkt. Mgufuli

Aidha, Rais Magufuli ameishukuru Benki ya Dunia kwa kutoa fedha za ujenzi wa mradi huo na kuitaka kampuni ya (CCECC) kutoa ajira kwa wakazi wa eneo hilo, huku akiwasisitizia wananchi kulinda miundombinu ya mradi huo pindi utakapokamilika.

Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Jim Yong Kim ameipongeza serikali kwa kubuni mradi huo mkubwa kufanyika hapa nchini.

“Mradi huu pamoja na wa BRT utasaidia kubadilisha maisha ya wananchi hususani kwamba Tanzania ni nchi inayokuwa kiuchumi kwa kasi,” amesema Kim.

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply