RC Makonda azindua jengo la upasuaji katika Mwananyamala

126
0
Share:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda amezindua Jengo la Upasuaji katika Hospital ya Rufaa ya Mwananyamala yenye thamani ya zaidi ya milioni 420 inayoenda kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Jengo hilo la kisasa lenye ghorofa Moja limepewa jina la HON. PAUL MAKONDA OBSTETRIC THEATRE kama sehemu ya kuenzi jitiada za Makonda kuboresha sekta ya afya kwa kumtafuta mfadhili GSM Foundation aliekubali kujenga jengo hilo bila kutumia pesa ya Serikali.

Makonda aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo hilo mnamo Machi 13, 2016 siku ambayo ndio aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa na sasa jengo limekamilika likiwa na vyumba viwili vya upasuaji vyenye uwezo wa kufanya upasuaji kwa wakati mmoja na kuhudumia wagonjwa 20 kwa siku.

RC Makonda amesema kabla ya kujengwa kwa jengo hilo wagonjwa walikuwa wakisongamana kusubiri kufanyiwa upasuaji kitendo kilichokuwa kikisababisha maumivu makali na vifo vya mama na mtoto lakini kupitia jengo hilo vifo vinaenda kupungua.

Makonda ameishukuru GSM Foundation kwa kufanikisha ujenzi wa jengo hilo ambapo inakadiriwa hospitali ya Mwananyamala inapokea wagonjwa kuanzia 1,500 hadi 2,000 kwa siku na kati ya hao ni wajawazito wanaohitaji huduma ya upasuaji.

Amesema hadi sasa zaidi ya kinamama 55 wamejifungua salama ndani ya jengo hilo na linaendelea kupokea kinamama wajawazito kila kukicha.

Baadhi ya kinamama waliofanyiwa upasuaji wamemshukuru Makonda kuwajengea jengo la upasuaji linalowawezesha madaktari kufanya kazi yao pasipokuwa na usumbufu na wanafurahia kuona huduma za upasuaji zinaenda vizuri.

Viongozi waliohudhuriwa uzinduzi huo akiwemo Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Mstahiki Meya wa Kinondoni, watendaji wa Afya na wananchi wamempongeza Makonda kwa jitiada kubwa anazofanya kuboresha sekta ya afya Jijini Dar es salaam.

Share:

Leave a reply