RC Singida awapa majukumu mazito wakuu wa wilaya wapya

276
0
Share:

Mkuu wa mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe, amewatangazia kiama watumishi wa umma ambao wameanzisha kampuni binafsi ndani ya maeneo yao ya kazi na kuzitumia kujipatia fedha za umma, kitendo ambacho ni kinyume na mikataba yao.

Mkuu huyo wa mkoa aliwaagiza wakuu wapya wa wilaya aliowaapisha, watoe kipaumbele kuwabaini mapema watumishi wa aina hiyo ambao amewabatiza jina la ‘majambazi wa miradi ya maendeleo ya wananchi’.

Mhandisi Mtigumwe, alisema kuwa uchuguzi wa kina ufanyike wa kubaini watumishi wa aina hiyo waliofanya ujambazi huo siku za nyuma, na ambao wanauendeleza hadi sasa.

“Kwenye miradi ya wananchi inayotekelezwa na serikali, huko ndipo ujambazi wa kuchota fedha za umma ulikojaa. Miradi inatekelezwa chini ya kiwango au inatumia fedha nyingi za serikali nje ya kusudio,
“Watumishi waliohusika na ujambazi huo, na wale ambao wameshirikia kubariki ujambazi huo, wote kwa pamoja watambue kuwa siku zao za kufikishwa mbele ya vyombo vya kisheria, zinahesabika,” alifafanua.

Akisisitiza zaidi, aliwataka wakuu hao wa wilaya, wawe wakali sana wasimamie watumishi wa umma, wadumishe uadilifu, uaminifu, wafanye kazi kwa weledi na wanaopiga vitendo vya kuomba na kupokea rushwa.

Aidha, Mhandisi Mtigumwe aliwataka wakazisimamie halmashauri ziweze kukusanya mapato yake ya ndani kwa zaidi ya asilimia 80, ili ziondokane na hatari ya kufutwa.

“Niwaambie tu kwamba halmashauri zote za mkoa wetu, zina utamaduni wa kutokukusanya mapato yake ya ndani kwa asilimia 80 zilizowekwa na serikali.Kuanzia leo nendeni mkalisimamie hili kikamilifu, ili halmashauri ziwe na uwezo wa kutoa huduma na kugharamia miradi ya maendeleo ya wananchi,” alisema.

Amewataka pia waende kuhamasisha wananchi wejenge utamaduni wa kulipa kodi mbalimbali za serikali, na kwamba wasimamie pasiwepo tena kwa vizuizi vya aina yo yote barabarani.

Mkuu huyo wa mkoa, alitumia fursa hiyo kuwapongeza na kuwashukuru wananchi wa mkoani hapa kwa juhudi zao za kumaliza uhaba wa madawati zaidi ya 40,000 uliokuwepo.

Kwa upande wake mkuu mpya wa wilaya ya Ikungi, Miraji Mtaturu, pamoja na kumshukru rais Dk.Magufuli kwa kumwamini na kumteua kuwa mkuu wa wilaya, ameahidi hatamwangusha atatumia nguvu zake zote kuhakikisha wilaya hiyo, inabadilika kwa wananchi wake kujiletea maendeleo.

Naye mkuu wa wilaya ya Mkalama Injinia Masaka John Masaka, alisema kutokana na kuwa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, ana uzoefu utakao mwezesha kuwatumikia wananchi ipasavyo.

“Wananchi wa wilaya ya Mkalama ,kwa ushirikiano wao, nina uhakika tutafanya mambo makubwa ya maendeleo katika wilaya hiyo ambayo bado changa.Ila tu nitoe onyo kwa watumishi ambao hawatabadilika na kuacha ufisadi, nitasimamia sheria zinachukua mkondo wake dhidi ya watumishi wa aina hiyo,” alisema Injinia Masaka.

IMG_6821

Mkuu wa mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe (kulia),akimkabidhi nyaraka za miongozi ya kiutendaji, mkuu wa wilaya ya Iramba, Injinia Masaka John Masaka muda mfupi baada ya kumwapisha.

IMG_6823

Mkuu wa mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe (kulia) akimwapisha mkuu wa wilaya ya Singida Elias Choro Tarimo.

IMG_6827

Mkuu wa mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe (kulia), akimwapisha mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu. Hafla hiyo imefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa mjini hapa.

IMG_6837

Mkuu wa mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe (kulia), akimkabidhi nyaraka za miongozi ya kiutendaji, mkuu wa wilaya ya Iramba, Emmanuel Uhahula muda mfupi baada ya kumwapisha.

IMG_6840

Mkuu wa mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe, akizungumza muda mfupi baada ya kuapisha wakuu wa wanne wa wilaya za mkoani hapa. Pamoja na mambo mengine, Mtigumwe amewaagiza wakuu hao kuzingatia sheria,kanuni na taratibu wakati wote wanapotekeleza majukumu yao. Kushoto ni katibu tawala mkoa, Dk.Angelina Lutambi.

IMG_6850

Mkuu wa mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe (wa nne kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na wakuu wapya wa wilaya nne za mkoa huu baada ya kuwaapisha. Wa kwanza kulia (waliokaa)ni mkuu wa wilaya ya Iramba,Emmanuel Uhahula,mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu na katibu tawala mkoa wa Singida,Dk.Angelina  Lutambi. Kushoto wa kwanza ni mbunge wa jimbo la Singida mjini mwalimu Mussa Sima,mkuu wa wilaya ya Mkalama injinia Masaka John Masaka na mkuu wa wilaya ya Singida Elias Choro Tarimo.Waliosimama nyuma ni wakurugenzi, wenyeviti na mstahiki meya  wa halmashauri za wilaya na Manispaa ya Singida. (Picha na Nathaniel Limu)

Share:

Leave a reply