RC Tabora awataka wakulima kuacha starehe

80
0
Share:

Wakulima wa Pamba na mazao mengine Mkoani Tabora wametakiwa kutumia fedha zinazotokana na  mauzo ya mazao yao katika shughuli za kuendeleza  familia zao na kupanua shughuli zao za kilimo ili waweze kuondokana na kilimo cha kizamani na waendeshe shughuli zao kisasa.

Kauli hiyo imetolewa jana Wilayani uyui na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wkati wa ziara yake katika maeneo mbalimbali mkoani humo kuelimisha wakulima wa pamba juu ya unyunyuziaji sahihi wa zao hilo kwa ajili uya kuua wadudu waharibifu.

Alisema fedha wanazozipata ni vema wakazitumia kwa matumizi sahihi na mahitaji ya lazima badala ya kutumia fedha hizo kwa shughuli ambazo sio za msingi kama vile starehe, ulevi, shughuli za ushirikina ambazo kwa kiasi kikubwa zinawarudisha nyuma kimaendeleo na kuzifanya familia zao kuendelea kuishi maisha duni.

“Ndugu zangu najua mtapata fedha nyingi kwa kuwa mumelima pamba kwa wingi na vizuri …naomba tumieni fedha mtakazopata katika kujenga nyumba nzuri, kula vizuri, kusomesha watoto wenu, kuvaa nguo nzuri na ikibidi kununua vyombo vya usafiri kwa ajili ya matumizi ya familia zenu” alisema Mwanri.

Alisema kuwa fedha watakazopata ni vema pia zikawasaidia katika kuboresha kilimo chao na kukitoa katika hali ya kilimo cha mazoea cha kuzalisha mazao kwa ajili ya matumizi ya kila siku na kuingia katika uzalishaji ambao unampa mkulima ziada ambayo ndio itakayomwezesha kupata maendeleo.

“Tukitaka kufanikiwa ndugu zangu wakulima wangu wazuri ambao ninawapenda ni kulenga katika uzalishaji unaowapa ziada…bila ziada hakuna maendeleo…ziada ndio itawasaidia kuwa na fedha kwa ajili ya kununua mabati, ziada ndio itawasaidia kununulia simenti na vitu vingine kwa ajili ya kuboresha maisha yenu” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema ni jukumu la viongozi kuwatahadharisha wananchi ikiwemo wakulima kuwa na matumizi shaihi ya mapatao ya ili kujiletea maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tabora-Uyui Said Ntahondi aliwataka wanaume kuacha kutumia fedha wanazozipata kutokana na mauzo ya mazao bila kuwashirikisha wake zao kwa kuwa kufanya hivyo mara nyingine fedha zinaishia katika matumizi yasiyo sahihi.

Alisema pindi wanapopata fedha ni vema wakaweka vikao vya kifamilia ili kubaini vipaumbele vya matumizi ya fedha walizopata kabla ya kuanza kuzitumia ili ziweze kunufainisha watu wote katika familia.

Naye Mkulima kutoka Kijiji cha Muhuridede wilayani Uyui Helena Augustino aliwaomba wanaume kuzingatia ushauri wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora wa kupenda kukimbilia mijini pindi wanapokea fedha za mauzo na kujikuta zikimalizika katika anasa na starehe huko familia ikiendelea kutabika.

Alisema inapotea hali hiyo wanaopata shida ni wanawake na watoto ambao kwa kiasi kikubwa ndio wanaoshiriki katika shughuli za shamba.

Na Tiganya Vincent

Share:

Leave a reply