Ripoti ya TWAWEZA: CCM yaimarika, CHADEMA yaporomoka

597
0
Share:

Ripoti ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Twaweza, inaonyesha kuwa CCM inakubaliwa na wananchi kwa asilimia 63, wakati kukubalika kwa Chadema kukishuka kutoka 32% ilivyokuwa 2013 hadi 17% mwaka huu, huku CUF ikishuka kutoka 4% hadi 1%. vilevile idadi ya watu wasikuwa na ukaribu na chama chochote ikipanda kutoka 5% hadi 17%.

Wakati akisoma matokeo ya ripoti hiyo leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji Twaweza, Aidan Eyakuze amesema CCM inakubaliwa zaidi na wazee kwa 80% ukilinganisha na 55% ya vijana, pia wanawake wanaikubali kwa 68% kuliko wanaume wanaoikubali kwa 58%. Huku maeneo ya vijijini ikukubalika zaidi kwa 66% kuliko mijini 57.

Kwa upande wa Chadema, Eyakuze amesema inakubalika zaidi miongoni mwa wanaume, vijana, matajiri na wenye kiwango kikubwa cha elimu.

Baadhi ya wanasiasa waliohudhuria katika uzinduzi wa Ripoti hiyo uliofanyika leo Juni 15, 2017 jijini Dar es Salaam, wametoa maoni yao juu ya sababu zilizopelekea vyama vya upinzani kupoteza mvuto kwa wananchi.

Katibu wa Itikadi na Uenezi ACT-Wazalendo, Ado Shaibu ameeleza kuwa, sababu ya Chadema kupoteza idadi ya wananchi wanaokikubali ni, kubanwa kwa shughuli za vyama vya upinzani ikiwemo zuio la mikutano ya kisiasa.  

“Chadema kimedondoka, ACT tumebaki palepale. Kwa nini vyama vya upinzani vimedondoka NI kwa sababu CCM inafanya siasa wakati vyama vya upinzani vimebanwa havina nafasi ya kujipambanua na kupambana na CCM inayoendelea kufanya siasa,” amesema.

Naye Ndelakindo kessy kutoka chama cha NCCR-Mageuzi amesema kuporomoka kwa vyama vya upinzani kumesababisha na viongozi wa vyama hivyo kukosa uhuru wa kujieleza na kufanya shughuli za kisiasa wakati CCM ikiendelea kufanya siasa kwa wananchi.

“Kuhusu umaarufu wa vyama vya siasa. Vyama vya siasa vimefungwa mdomo, havina uhuru wa kujieleza. Vyama vya siasa havihudumii wananchi tofauti na ilivyo kwa CCM ambayo ianendelea kufanya shughuli zake za kisiasa kwa wananchi, na ndiyo sababu ya kukosa mvuto,” amesema.

Kwa upande wa Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole amesema, “Chama cha CCM mwakani kitakuwa kisafi, wachafu wengi sasa wako upinzani, ndiyo maana kinazidi kuwa na mvuto kwa wananchi.”

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply