Sakata la ruzuku CUF lachukua sura mpya, Bodi ya Wadhamini yafunga akaunti kwa muda

878
0
Share:

Licha ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) wa wilaya saba za mkoa wa Mwanza hivi karibuni kulalamika kufungiwa akaunti za za benki za chama hicho ngazi ya wilaya na kupelekea kushindwa kufanya shughuli za chama hicho ikiwemo ujenzi wake.

Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma, Mbarala Maharagande amesema Bodi ya Wadhamini CUF yenye wajumbe toka pande zote mbili Bara na Visiwani imechukua uamuzi wa kuzifunga kwa muda  akaunti zote nchini kwa ngazi ya wilaya, kata na matawi ya chama kwa madai kuwa ni kutokana na wizi wa fedha za ruzuku uliofanywa na Profesa Ibrahim Lipumba , Mwenyeiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na wenzake.

Maharagande ameyasema hayo leo, wakati akitolea ufafanuzi wa malalamiko hayo, ambapo amesema fedha za ruzuku zilichukuliwa kinyume cha sheria pasipo kushirikishwa Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sheriff Hamad.

“Nyote mnafahamu kuwa kwa mujibu wa katiba ya CUF ukurasa wa 85 Ibara ya 93 (1) (a-k) (2) imempa Katibu Mkuu wa Chama majukumu ya kuhakikisha kuwa; “Atakuwa Mtendaji Mkuu wa Chama na pia mwajibikaji mkuu wa shughuli zote za utendaji za Chama kitaifa” pia “Atakuwa mwajibikaji mkuu wa mambo yote ya fedha na mali za Chama katika ngazi ya Taifa (Chief Accounting Officer),” amesema.

Aidha, Maharagande amesema kuwa, akaunti hizo zitafunguliwa na kutumiwa fedha za ruzuku za wilaya kama ilivyokuwa awali, baada ya  ruzuku kurejeshwa katika utaratibu wa kikatiba.

Hata hivyo, amedai kuwa, viongozi hao wa wilaya za Mwanza, wanawatambua viongozi waliopo ofisi kuu ya CUF Buguruni ambao walichukua ruzuku ambapo baadhi yao wamesimamishwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa  na kwamba maamuzi yote wanayofanya kwa nafasi hizo ni haramu na batili kwa mujibu wa katiba ya CUF.

“Tumepokea taarifa ya tamko la kikao cha viongozi wa mkoa wa Mwanza lililotolewa tarehe 15/02/2017 na kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari. Wakilalamika kufungiwa kwa akaunti zao za wilaya na Bodi ya wadhamini ya CUF. Kikao hicho cha viongozi wa Wilaya (7) za mkoa wa Mwanza, kutoka wilaya ya Nyamagana, Ilemela, Sengerema, Ukerewe, Kwimba, Magu Na Misungwi Kilichohudhuriwa Na Viongozi 10 ambao wameeleza kuwa wana nia ya kujenga, kulinda na kufufua upya chama cha wananchi (CUF) ambao kwa umoja wao wametoa taarifa hiyo,” amesema na kuongeza.

“Kikao cha viongozi wa wilaya saba wa Mkoa wa Mwanza kimefanyika kwa mujibu wa Ibara ipi ya katiba? CUF haina ngazi ya uongozi wa Mkoa kikatiba. Lakini hata hivyo, Viongozi kumi mliokutana mnaweza kupata uhalali wa kuwaamulia wajumbe wa Kamati za Utendaji za wilaya zenu 7 wapatao 189?”

Amesema kuwa, Bodi ya wadhamini ya CUF tayari imeshachukua hatua stahiki kushughulikia wizi wa fedha za ruzuku ya chama hicho katika mamlaka zinazohusika.

Share:

Leave a reply