“Serikali haitawafumbia macho Wezi wa kazi za Sanaa”- Dkt Mwakyembe

766
0
Share:

Serikali imesema itaendelea kuwachukulia hatua wote watakaobainika kusambaza kazi za sanaa kinyume na utaratibu ili kuondoa kero ya muda mrefu ya wizi wa kazi za Sanaa uliolalamikiwa na wasanii wote hapa nchini.

Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Dkt. Harrison Mwakyembe alipokuwa akizindua Kampuni ya Tyeeo Barazani Entertainment itakayohusika na usambazaji wa kazi za Sanaa kuanzia kesho.

“Serikali haitaendelea kuwafumbia macho wezi wa kazi za Sanaa,tutawashughulikia kama ambavyo tumeanza na mafanikio yameanza kuonekana yeyote anaetaka kusambaza kazi hizi aende Barazani Entartainment watamsaidia.” alisema Dkt. Mwakyembe.

Aidha amewataka wasanii wote hapa nchini kutumia Kampuni hiyo kwa manufaa ili waweze kupiga hatua ambapo pia amewahakikishia kuwa ndani ya kipindi kifupi kijacho sekta ya Sanaa itakuwa na mageuzi makubwa.

Kwa upande wake Katibu wa Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo amewahakikishia wasanii hao kuwa Maafisa Utamaduni wa Mikoa na Wilaya wapo tayari kushirikiana na Kampuni ya Barazani Entartainment katika kuleta mafanikio ya kazi zao.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Bw.John Kalaghe ameishukuru Serikali kwa ushirikiano ilioupatia kampuni hiyo tangu ilipoanzisha wazo hilo ambalo limefanikiwa na wasanii wataanza kunufaika na kazi zao kwani Kapuni hiyo itasambaza kazi zao kwa urahisi na salama zaidi.

Kampuni ya Tyeeo Barazani Entartainment itakuwa ndio wakala wa kusambaza kazi za sanaa ikiwemo Filamu za nje na ndani,Muziki,masomo ya watoto,na makala za kielimu kupitia simu ya mkononi kwa mitandao yote kwa malipo nafuu.

Na Shamimu Nyaki-WHUSM

Share:

Leave a reply