“Serikali ipo tayari kugharamia matibabu ya Lissu”- Waziri Ummy Mwalimu

393
0
Share:

Serikali imesema ipo tayari kugharamia matibabu ya Mbunge wa Jimbo  la Singida Mashariki
 Tundu Antiphas Lissu  ambaye kwa sasa hivi yupo Jijini Nairobi kwa matibabu kufuatiwa
shambulio alilolipata Septemba 7, mwaka huu Mkoani Dodoma.

Hayo yamesemwa Jijini Tanga na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Ummy Mwalimu wakati akiongea na waandishi wa habari kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.

Waziri Ummy Mwalimu alisisitiza  Serikali inasubiri kupata maombi kutoka kwa familia ya
mgonjwa ikiambatana na taarifa rasmi kutoka kwa  madaktari kuhusu mahitaji ya matibabu zaidi
 ya mgonjwa ”Serikali ipo tayari  kugharamia matibabu  zaidi ya Mhe.Lissu popote Duniani”.

Akiwa kama Mtanzania na Mbunge,Serikali inayo wajibu wa kugharamia matibabu yake hadi
apone ili aweze kuendelea na kazi ya kuwahudumia Watanzania na wana Singida Mashariki.

Serikali  inapenda kusisitiza kwamba iko tayari kuendelea kushughulikia matibabu endapo
maombi ya kufanya hivyo yatawasilishwa rasmi Serikalini,ikiwemo kupata taarifa ya maendeleo
ya afya yake kutoka kwa Madaktari wanaomhudumia hapo Nairobi ambayo itatakiwa kupatikana
kupitia ridhaa itakayotolewa na Mhe. Lissu au Mwanafamilia wa karibu kama taratibu za
Kidaktari zinavyoelekeza.

Aidha, Serikali imeshangazwa na dhana ya kuchangishana kwa ajili ya matibabu ya Mhe. Lissu,
kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kutokea matapeli watakaochangisha Watanzania fedha kwa
madai kwamba Mbunge huyo amekosa hela za matibabu.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anawashukuru Madaktari na
watoa huduma wote wa Hospitali ya Rufaa Dodoma kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya
katika kuokoa maisha ya Mhe.Lissu na kumtakia apate nafuu haraka

Na Nsachris Mwamwaja, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Afya,

Share:

Leave a reply