Serikali uaridhia mwekezaji kumilikishwa ardhi Msoga

223
0
Share:

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi ameridhia mwekazaji kupewa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda kijijini Msoga, Wilayani Chalinze, Mkoa wa Pwani.

Waziri Lukuvi amesema kuwa wanakijiji wana uwezo wa kutoa ardhi hadi ekari hamsini tu zaidi ya hapo ni Mhe. Rais mwenye uwezo wa kutoa hati kwa mwekazaji, hivyo alikwenda Msoga kujiridhisha kabla ya kumshauri Rais kutoa hati kwa mwekezaji.

Aliwauliza wananchi katika mkutano uliofanyika kijijini Msoga kama walikubaliana kumruhusu mwekazaji wa Region Recycling East Africa Limited kujenga kiwanda kijijini hapo, nao wananchi kwa pamoja walisema kuwa ndiyo walitoa ardhi yao kwa ajili ya uwekezezaji huo.

Baada ya kuhakiki, Mhe. Lukuvi aliahidi kwenda kumshauri Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kutoa hati kwa ajili ya mwekazaji huyo kutoka Kenya ili ajenge kiwanda ambacho kitatoa ajira kwa watu wa Msoga kati ya 40 na 100.

Kiwanda hicho kitakuwa kinatumia betri mbovu za gari na za umeme jua (Recycling) kama malighafi ya kutengeneza betri nyingine kwa ajili ya matumizi ya magari na mitambo ya umeme jua. Mwekezaji huyo alipewa jumla ya ekari 56 na wanakijiji wa Msoga kwa ajili ya uwekezaji huo.

Awali, Mhe. Lukuvi alisikiliza na kutoa suluhisho ama ufafanuzi kwa watu waliokuwa na migogoro ya ardhi ili kuwaondolea kero walizokuwa wakizipata kutokana na changamoto hizo.

Waziri Lukuvi alitumia muda huo kuwashauri wenyeviti wa vijiji ambavyo vina sura ya kimji kama Msoga kupandishwa hadhi na kuwa miji midogo. Kwa kufanya hivyo vijiji vitapimwa na kupangwa vizuri na wakazi wa maeneo hayo watapatiwa hati za umiliki wa miaka 99.

“Vijiji vilivyopimwa kimji vitaiingizia Serikali mapato na wananchi pia watapata fursa za kupata mikopo kwenye mabenki na kufanya biashara kubwa,” alisema Lukuvi na kuongeza kuwa anazishauri Halmashauri zote nchini kupandisha hadhi vijiji vya namna hiyo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Chalinze, Mhe. Ridhiwan Kikwete alimshukuru Mhe. Lukuvi kwa kuridhia umilikishwaji wa ardhi kwa mwekezaji kwani kiwanda hicho kikianza kazi kitatoa fursa mbalimbali zitakazochangia kuinua uchumi wa wakazi wa Msoga na maeneo ya jirani ikiwemo ajira.

Alimwomba Mhe. Lukuvi kupitia wizara yake kuwasaidia katika upimaji wa maeneo ya Chalinze kwani wao hawana uwezo wa kujipimia au kulipia gharama za upimaji.

Hatua za umilikishwaji ardhi kwa mwekezaji huyo, zilianza mwaka 2012 na kukamilika hivi karibuni kwa jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imekuwa karibu sana na wananchi kuwatatulia kero na changamoto mbalimbali.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi chini ya uongozi wa Mhe. William Lukuvi imetatua migogoro mingi ya ardhi hapa nchini na kuwafanya wananchi waishi kwa Amani katika maeneo yao.

Jonas Kamaleki- MAELEZO

Share:

Leave a reply