Serikali yaombwa kuongeza somo la kodi mashuleni

372
0
Share:
Serikali  imeombwa kuangalia uwezekano wa kuingiza suala la kodi katika mtaala wa elimu nchini ili ianze kufundishwa kuanzia shule za msingi hadi kwenye vyuo vikuu.
 
Lengo la hatua hiyo,ni kujenga kizazi cha Watanzania wanaoelewa juu ya umuhimu kulipa kodi mbalimbali na kujua faida zake.
 
Wakiisha kutambua umuhimu huo na faida zake, bila kushurutishwa watakuwa mstari wa mbele katika kulipa kodi zilizobainishwa na serikali.
 
Hayo yamesemwa juzi na meneja wa shirika la ActionAid Tanzania, Karoli Kadeghe,wakati akitoa taarifa yake kwenye ufunguzi wa  mafunzo juu ya uhamasishaji wa haki za mtoto shuleni, na usawa katika kulipa kodi. Hii ni katika  kuboresha makusanyo ya ndani yaweze kugharamia utoaji elimu bora kwa motto wa kike-Tanzania.
 
Akisisitiza, Karoli alisema upo umuhimu mkubwa kwa serikali kuingiza suala hilo katika mtaala wa elimu, ili kujenga kizazi cha wazalendo wanaojua na kuzingatia umuhimu wa kulipa kodi.
 
“Kwa njia hii ya kuwa na kizazi cha wazalendo wa kweli, ambao watakuwa na utayari wa kulipa kodi kwa wakati,tutaijengea serikali uwezo wa kuboresha zaidi,huduma za kijamii zikiwemo za sekta ya elimu. Na pia kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi,” alisema.
 
Akisisitiza zaidi, Karoli alisema kodi zikilipwa ipasavyo, serikali itakuwa na uwezo  mzuri wa kuboresha miundo mbinu katika shule za msingi. Hali hiyo, itavutia wanafunzi wakiwemo wa kike kujisomea kadri ya uwezo wao.
 
“Hivi sasa miundo mbinu ikiwemo ya vyoo katika shule nyingi za msingi,ni mibovu kupindukia.Hali hii inatokana na serikali kuwa na uwezo mdogo.Uwezo huu mdogo,unasababishwa na vitendo vya ukwepaji kodi na misamaha ya kodi,” alisema.
 
“Ndugu washiriki wa mafunzo haya,pamoja na serikali kushindwa kutoa asilimia mia moja ya fedha za kutekeleza bajeti (elimu) ya 2016/2017,tafiti zinaonyesha kuwa Tanzania inapoteza fedha nyingi kupitia misamaha ya kodi,” alifafanua Karoli.
 
Alisema upotevu wa kodi,unachangia elimu kuwa duni kwa wanafunzi wakiwemo wa kike.Pia ni chanzo cha walimu kutokulipwa stahiki zao kwa wakati.
 
“Ili kuhakikisha tunakuwa na fedha za kutosha kugharamia elimu yetu,ni lazima kuimarisha vyanzo vya mapato yetu. Kila mtu anayepaswa kulipa kodi, alipe kodi.Ni lazima tuondokane na utegemezi toka kwa wahisani,” alisema.
 
Akieleza madhara ya utegemezi, Karoli alisema bajeti ya elimu 2016/2017, takribani shilingi 277 bilioni sawa na asilimia 31, ilitarajiwa kukusanywa kutoka kwa wahisani.
 
“Hata hivyo,hadi kufikia machi 2017,wahisani walikuwa wametoa shilingi 132 bilioni sawa na asilimia 47.6. Ni vema serikali iimarishe vyanzo vyake vya mapato ya ndani,ili kuepuka aibu hii.Sisi wadau wa elimu tunalo jukumu la kuisimamia serikali katika kutimiza wajibu wake,” alisema.
 
Mafunzo hayo ambayo yaliandaliwa kwa pamoja na shirika la mtandao wa elimu Tanzania (TEN/MET), ActionAid Tanzania na shirika la maendeleo ya elimu Singida-MEDO, kwa ufadhili wa NORAD, yalifanyika kwenye ukumbi wa mikutano kanisa katoliki mjini hapa.
 
Mafunzo hayo yalihudhuriwa na wanachama wa chama cha walimu Tanzania (CWT) mkoa wa Singida na viongozi kutoka asasi za kiraia.
Na Nathaniel Limu, Singida
Share:

Leave a reply