Serikali yataja sababu ya kufanya maboresho mara kwa mara ya kanuni

191
0
Share:

Serikali imesema kasi kubwa ya maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano ambayo imeikumba sekta ya habari inalazimu jamii kufanya maboresho ya mara kwa mara ya Sera na Kanuni ili kuepusha matumizi mabaya ya vyombo vya habari.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel amesema kuwa katika kufanya hivyo ni wajibu wa wadau wote kushirikiana kutumia vyema maendeleo hayo ya tekinolojia kwa ajili ya ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa.

Profesa Elisante alisema hayo leo wakati akifungua mkutano wa siku moja wa mashauriano miongoni mwa wadau wa sekta ya habari kuhusu mapendekezo ya Kanuni za maudhui yanayorushwa na vituo vya Utangazaji vya Redio na Televisheni na Kanuni za Maudhui Mtandaoni.

“Ni wajibu wetu kama taifa linalosimamia maadili na ambalo lingependa kudumisha amani na
mshikamano, kutunga kanuni ambazo zitahakikisha kuwa kunakuwa na matumizi mazuri, sahihi
na salama ya maudhui ya mtandaoni,” alisisitiza Profesa Elisante.

Aliwaambia washiriki wa mkutano huo kuwa kuweka kanuni ni suala muhimu na kuwakumbusha
matumizi ya mfumo wa habari mtandaoni wakati mwingine umetumika kupotosha jamii, kujenga
chuki, kutoa habari za faragha za watu binafsi au habari zilizoleta sintofahamu miongoni mwa
jamii.

Aliongeza kuwa kufanyika kwa mkutano huo ni jambo muhimu kwa kuwa washiriki watapata
fursa ya kujadili kanuni hizo ambazo baadhi zinadaiwa kuwa zimepitwa na wakati na pia
haziendani na utendaji na kazi katika ushindani wa soko.

Katika mkutano huo ambao Profesa Elisante alikuwa mwenyekiti wake alieleza kuwa pamoja na
kuwa bado kumekuwepo na mijadala mikali katika nchi nyingi zikiwemo za Magharibi kuhusu
uwekaji kanuni lakini ukweli unabaki kuwa nchi hizo zimeweka sheria na kanuni zinazosimamia
matumizi ya intaneti.

“Ni kweli kwamba tekinolojia hii ina changamoto katika usimamizi lakini hakuna uhuru usio na
mipaka. Kwa hiyo imekuwa ni wajibu wa kila nchi kutafakari mahitaji na umuhimu wa kutoa
miongozo itakayosaidia jamii na taifa,” alieleza Profesa Elisante.

Mapema akimkaribisha Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali Dk. Hassan Abassi aliwaeleza washiriki kuwa Mkutano huo ni muhimu katika historia ya maendeleo ya tasnia ya habari nchini kuwa umelenga kuweka kanuni bora zitakazoratibu tasnia.

“Tumeitana hapa kushauriana kuhusu kanuni hizi hivyo hakuna haja ya kueneza wasiwasi kuwa
katika mitandao ya kijamii kuwa serikali imedhamiria kudhibiti vyombo vya habari” Dk. Abbassi
aliwaeleza washiriki.

Wakati huo huo, Serikali imeongeza muda wa siku saba kwa wadau wa sekta ya utangazaji na mitandao kuwasilisha maoni yao kuboresha kanuni zilizopendekezwa. Uamuzi huo umefikiwa mwishoni mwa mkutano wa mashauriano kujadili kanuni hizo ambapo wadau wengi waliomba muda zaidi.

Akifunga mkutano huo Profesa Elisante alisema ni vyema wadau wakaitumia fursa hiyo kuwasilisha maoni yao kwa maandishi ili kuboresha kanuni hizo hatimae taifa kuwa na kanuni bora kwa faida ya jamii yote.

Katika maelezo yake kufunga mkutano huo Profesa Elisante aliwashukuru washiriki kwa kutoa maoni yao na kuahidi kuwa serikali itayafanyia kazi maoni hayo.

Alieleza kuwa ni ukweli kuwa vyombo vya habari vinafanya biashara na pia vina wajibu wa kuelimisha jamii hivyo vitu viwili havina budi kwenda sambasamba bila kuathiri upande mwingine.

Na Pascal Dotto, MAELEZO

Share:

Leave a reply