Serikali yatoa ufafanuzi kuhusu kuwepo kwa taarifa kuwa imeshusha mishahara ya madaktari

344
0
Share:

Serikali imesema kuwa haijashusha mshahara wa madaktari kama inavyodaiwa na habari zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii kuwa imeshuka kwa asilimia 30% ili kuendana na dhana ya hapa kazi tu na kwamba imekusudia kufuta malipo ya posho za wataalamu wa afya walio katika mafunzo kwa vitendo ufafanuzi kwa umma wa watanzania na watumishi wa sekta ya afya kuwa.

Kutokana na Taarifa aliyoitoa Katibu Mkuu (Afya) alipokuwa anaongea na Watumishi wa Hospitali ya Bugando ililenga kutoa ufafanuzi kwa Watumishi wa Hospitali hiyo kuhusu kufutwa kwa kibali cha Msajili wa Hazina kilichowawezesha watumishi wa Hospitali hiyo kulipwa Mishahara ya Taasisi zilizo chini ya Msajili wa Hazina tangu mwaka 2012 na kusema taarifa hizo siyo za kweli.

Aidha,Taarifa hiyo ilisema kuwa ieleweke kuwa mishahara ya Watumishi wa Sekta ya Afya haizingatii ngazi ya Vituo vya kutolea huduma kama vile Zahanati, Kituo cha Afya, Hospitali, au Hospitali za Rufaa bali huzingatia uzito wa kazi na majukumu ya kada husika. Hivyo, mshahara wa Daktari wa Hospitali ya Wilaya ni sawa na ule wa Hospitali ya Rufaa ngazi ya Mkoa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa kumekuwa na Uvumi kuwa Serikali inakusudia kufuta posho ya ‘Interns’ kuanzia mwaka huu wa fedha hivyo jambo hilo sio sahihi kwa kuwa hakuna chombo chochote cha Serikali ambacho kimetoa maamuzi hayo.

Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa ajira mpya kwa mwaka 2015/2016 ufafanuzi ulitolewa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba hakutakuwa na waajiriwa wapya hadi hapo Zoezi la Uhakiki wa Watumishi Serikalini litakapokamilika. Hivyo, vibali vya ajira vilivyokuwa vimetolewa vimefutwa hadi hapo itakapotamkwa vinginevyo.

Mbali na hayo taarifa hiyo inasisitiza kwamba maamuzi ya Serikali hutolewa na Mamlaka husika kwa nyaraka. Hivyo, watumishi wa Sekta ya Afya na wananchi kwa ujumla wanaaswa kuzingatia taarifa zinazotolewa na Mamlaka za Serikali kuhusu Masuala yanayowahusu ambayo mara nyingi hutolewa kwa nyaraka badala ya Mitandao ya kijamii.

Share:

Leave a reply