Serikali yawabebesha mzigo wazazi na walezi

358
0
Share:

Serikali imetoa rai kwa wazazi wote nchini kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa watoto ikiwemo kuwapatia malezi bora na kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili ili waweze kukua vyema na kulisaidia taifa hapo baadae. 

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Sihaba Nkinga wakati akizungumza kwenye kipindi cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na kituo cha Televisheni TBC 1.

Nkinga alisema kuwa ni jukumu la wazazi au walezi kuhakikisha watoto wanapata mahitaji yote ya msingi kama vile chakula, malazi, elimu pamoja na ulinzi ili waweze kuwa salama katika mazingira wanayoishi na yanayowazunguka.  

“Mzazi au mlezi anapaswa kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mtoto na kumlinda dhidi ya ukatili kwani imebainika kuwa kwa kiasi kikubwa ukatili wa watoto unaanzia kwenye familia,” alifafanua Nkinga. 

Aidha amewataka baadhi ya wanajamii kuacha kumaliza kesi za ukatili kwenye ngazi ya familia badala yake watoe taarifa polisi pindi watoto wanapofanyiwa vitendo vya ukatili iwe kupigwa, kubakwa au kulawitiwa ili wahusika waweze kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Alieleza kuwa kwa mwaka 2016 kuna ongezeko la asilimia 31 kwenye utoaji taarifa za matukio ya ukatili kwa watoto lakini bado uhamasishaji unaendelea ili matukio yote yawe yanaripotiwa na sheria ichukue mkondo wake.

“Wazazi wawe wanatoa taarifa haraka kwenye vyombo husika kwani matukio ya ukatili kwa watoto yanawaathiri kiafya, kisaikolojia na hata kupelekea vifo.”  

Akizungumzia juhudi za Serikali, Nkinga alisema kuwa jitihada mbalimbali zinafanyika kukomesha ukatili kwa watoto na Serikali inafanya mapitio ya baadhi ya kanuni za Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambazo zimepitwa na wakati.

Akifafanua kuhusu Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Ukatili wa Watoto na Wanawake uliozinduliwa mwaka 2016 alisema umelenga kuwapatia elimu watoto wa kike na Serikali itashirikiana na wadau wa elimu ili mtoto wa kike aweze kusoma katika mazingira bora na salama.

Aidha Nkinga alisema kuwa pamoja na uwepo wa Dawati Maalum la Watoto kwenye vituo vya Polisi, Serikali ina mkakati wa kuweka Dawati la Ulinzi na Usalama katika shule za Msingi na Sekondari kote nchini ili watoto waweze kupata elimu ya kujilinda na kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa vitendo vya ukatili.

Na Fatma Salum (MAELEZO)

Share:

Leave a reply