Serikali yaweka mikakati mipya ya kupunguza vifo vya kina mama na watoto

622
0
Share:

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametaja mikakati minne itakayosaidia kupunguza vifo vya kina mama na watoto vitokanavyo na uzazi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa miaka minne wa wizara hiyo uliolenga kupunguza vifo hivyo kwa asilimia 30 kutoka vifo 432 hadi 392 kwa vizazi hai laki moja ifikapo mwaka 2020.

Ummy ameeleza mikakati hiyo, leo Aprili 20, 2017 jijini Dar es Salaam, katika Kongamano la Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Kina Mama ya Uzazi lililohusisha madaktari bingwa kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujadili namna ya kupunguza vifo hivyo.

Amesema, sababu nyingine ya vifo hivyo ni, matumizi madogo ya huduma za uzazi wa mpango kwa kina mama ambapo takwimu zinaonyesha kuwa, kati ya wanawake 100, 32 pekee ndio huipata huduma hiyo, na kwamba mkakati wake ni kusogeza karibu huduma hiyo kwa wananchi hasa walio vijijini, ambapo wizara yake katika bajeti ya 2017/18 imetenga fedha zake kwa ajili kuondoa changamoto zinazokwamisha huduma hiyo kufikia wanawake wengi.

Mkakati wa pili alioutaja, ni kuboresha huduma na miundombinu ya vituo vya afya ikiwa pamoja na ujenzi wa vyumba vya upasuaji, wodi za wazazi na maabara za damu ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa huduma bora za afya ya uzazi, inayosababisha kina mama wengi na watoto kupoteza maisha.

“Nashukuru tumepata fedha kutoka Benki ya Dunia, tutahakikisha tunaboresha vituo vya afya 100 ambavyo tumeanza kuvifanyia tathimini, pamoja na kujenga benki za damu tano katika mikoa 5. Pia tumepanga kuhamasisha kina mama kutumia uzazi wa mpango,” amesema.

Mkakati wa tatu alioutaja, ni uongezaji wataalamu wa afya na wauguzi katika vituo vya afya, hospitali za wilaya na mikoa ili kuondoa changamoto ya kina mama kujifungua pasina kupata huduma kutoka kwa wataalamu wa afya, ambapo kwa sasa asilimia 64 pekee ya wanawake wanaojifungua nchini, ndio wanaopata huduma hiyo.

“Serikali hivi karibuni imetangaza kuajiri madaktari 258, watalaamu 209 wataenda TAMISEMI wakapangaiwe vituo vya afya na hospitali za wilaya na mikoa, wengine watapelekwa katika hospitali kubwa. Tutaendelea kuajiri wauguzi na kuongeza wataalamu ili kuhakikisha huduma bora ya afya ya uzazi inawafikia kina mama wote na kupunguza vifo,” amesema.

Amesema, serikali itawachukulia hatua wakurugenzi wa halmashauri watakao shindwa kutekeleza majukumu yao kwa kuboresha huduma za afya katika hospitali husika na vituo vya afya, ikiwa ni mkakati wa nne wa kutokomeza vifo hivyo.

“Bado huduma katika ngazi ya vituo vya afya, hospitali za wilaya na mikoa si nzuri sababu ya kina mama wengi kukimbilia Muhimbili, kila Mkurugenzi wa Halmashauri ahakilishe anaboresha huduma ya afya ya uzazi na tutawachukulia hatua wakurugenzi wasiotekeleza majukumu yao. Sababu vifo vitokanavyo na uzazi vinaepukika kwa uwepo wa huduma bora za afya,” amesema.

Kwa upande wa Kongamano hilo, Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Kina Mama ya Uzazi Tanzania (AGOTA), Profesa Andrea Pembe amesema madaktari hao wataongeza juhudi zaidi ili kurahisisha utekelezaji wa mpango mkakati uliopo wa kupunguza vifo hivyo.

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply