Serikali yazindua mwongozo wa huduma za maji na Usafi wa mazingira

204
0
Share:

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto  imezindua mwongozo wa huduma za maji na usafi wa mazingira katika vituo vya tiba ikiwemo zahanati, vituo vya afya na hospitali ikiwa ni katika kuelekea uzinduzi wa awamu ya pili ya  kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira iitwayo NIPO TAYARI.

Akiongea wakati wa uzinduzi huo Mkurugenzi wa Sekta Ofisi ya Rais Tamisemi, Dkt. Andrew Komba amesema uzinduzi wa mwongozo huo ni katika kueleka awamu ya pili ya kampeni ya NIPO TAYARI itakayozinduliwa rasmi na Makamu wa Rais,Mhe.  Samia Suluhu Hassan ifikapo Desemba 7 mjini Dodoma.

“Mwongozo huo utasimamia na kutekeleza shughuli zinazohusiana na mazingira na umelenga katika kutoa maelezo stahiki namna ambavyo vituo vya afya, ikiwemo ngazi za chini mpaka juu ili maelekezo hayo yaweze kutumika katika upangaji wa mipango na uandaaji wa bajeti zitakazotumika,” amesema Dkt. Komba.

Aidha,Dkt. Komba amesema kuwa watanzania tunatakiwa kuzingatia usafi wa mazingira pamoja kutumia vyoo bora ili kuweza kudumisha afya njema kwa maendeleo ya Tanzania.

Kwa upande wake  Mratibu wa Kampeni ya Kitaifa ya Usafi ya Mazingira, Anyitike Mwakitalima amesema kuwa kampeni hiyo inalenga kuwahamisha wananchi kuweza kutumia vyoo bora na mpaka kufikia Juni  2021 kaya zote nchini  ziwe zinatumia vyoo.

“Kutokana  na kulegalega  katika baadhi ya maeneo, waligundua kwamba kisababishi kimojawapo ilikuwa ni ukosefu wa mwongozo wa taifa ambao wadau na serikali ingeutumia kusimamia usafi wa mazingira kwahyo kampeni hii itahakikisha mpaka kufikia 2025 kaya zote zinatumia vyoo vilivyo bora” alisema Bw. Anyitike.

 Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mipango kutoka Shirika la Water Aid, Abel Duganga amesema kutokana na kukosekana kwa mwongozo huo unaopima hali ya maji nchini utendaji wa serikali na wadau ulikuwa ukisuasua,  lakini sasa utawezesha kuwa na vigezo vinavyofanana katika kupima na kuwa na takwimu sahihi.

 

Share:

Leave a reply