Singida United yaomba msaada wa fedha kwa MO Dewji

338
0
Share:

Mwenyekiti wa klabu ya soka ya Singida United, Yusuph Mwandami, ametoa wito kwa wazawa wa mkoa wa Singida, kuisaidia kwa hali na mali timu yao hiyo ili iweze kushiriki ligi daraja la kwanza bila matatizo.

Mwandami ametoa wito huo juzi wakati akizungumza na blog ya MO, juu ya maandalizi ya timu hiyo itakayoshiriki ligi daraja la kwanza inayotarajia kuanza kutimua vumbi Septemba, 24 mwaka huu.

Alisema kazi ya kuendesha timu ya soka, ina mahitaji mengi makubwa ikiwemo gharama mbalimbali.

“Kwa kifupi tu, ni kwamba hakuna starehe yoyote au burudani isiyohitaji gharama. Kwa muda mrefu, binafsi nimebeba mzigo wote hadi timu ikapanda daraja la kwanza. Sasa tunapigania mkoa urejeshe heshima yake kwenye mchezo wa soka, na hilo litafanikiwa endapo kila mwana Singida atachangia timu yake”,, lisema mwenyekiti huyo.

Akisisitiza zaidi, Mwandani ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi (CCM) mkoani hapa,amewaomba wazawa waliopo ndani na nje mkoa akiwemo aliyekua mbunge wa jimbo la Singida mjini, Mohamed Dewji MO, kuiombea na kuichangia timu yao.

“Tuna mawazo hapo baadaye timu yetu iwe kampuni ambayo wapenzi wa soka na wadau wengine watanunua hisa. Lengo ni kwamba timu iwe na uwezo wa kujiendesha yenyewe,” alifafanua zaidi.

Kwa mujibu wa msemaji wa Singida United, Elisante John, timu hiyo inayosaka tiketi ya kurejea ligi kuu,itaanza kutupa karata yake September 24 mwaka huu, itakapo ikaribisha na JKT Mgambo ya Tanga, kwenye uwanja wa Namfua.

Aidha, Elisante amesema Septemba, 31 mwaka huu, Singida United itaikaribisha pia Panoni F.C ya mkoa wa Kilimanjaro,kwenye uwanja wa Namfua mjini hapa.

Kwa upande wake kocha wa timu hiyo, Felix Minziro, alisema timu imejiandaa vizuri baada ya kuweka kambi jijini Dar es salaam na kucheza mechi sita za kujipima nguvu.

Minzoro amewataka wakzi wa mkoa wa Singida ‘kuisapoti’ timu yao na kufika wingi uwanja wa namfua, kuishangilia timu yao inapocheza mechi za nyumbani, ili iweze kushinda.

Na Nathaniel Limu, Singida

Share:

Leave a reply