SIRVICONET waendesha mradi wa kumwezesha mwanamke kumiliki ardhi Singida

226
0
Share:

Sheria za Ardhi za Tanzania zinaeleza wazi kwamba haki ya mwanamke katika kupata Ardhi,kumiliki,kutumia na kuuza ni sawa na kwa kiwango kilekile kama ilivyo kwa mwanaume.

Hivyo kwa sheria hiyo kama inavyoweka bayanaa uhalali wa umiliki kwa mwanamke,hivyo ni dhahiri kwamba mwanamke ana haki sawa na mwanaume katika kupata Ardhi,kumiliki kutumia kuuza na hata kuweka rehani sawa na mwanaume.

Kwa mujibu wa sheria za Ardhi za Tanzania,kamwe hazimnyimi mwanamke haki ya Ardhi isipokuwa mfumo wetu wa kijami,kisiasa na kiuchumi ndio ambao unamnyima mwanamke haki ya Ardhi.

Hata hivyo sheria inatoa haki ya Ardhi kwa mwanamke sawa na mwanaume,lakini sababu za kijinsia,kiutamaduni,kijamii na kiuchumi ndizo zinazomnyima mwanamke haki hizo kwani hazitoi fursa rafiki kwa mwanamke.

Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999 ambayo inatoa haki sawa kwa mwanamke na mwanaume katika kupata,kumiliki,kutumia,kuuza au kuigawa Ardhi,na kwamba sheria hiyo ya Ardhi inaeleza kwamba sheria yeyote ile ya kimila itakayokwenda kinyume kwa kuwanyima wanawake,watoto au watu wenye ulemavu uhalali wa kumiliki mali,kutumia au kupata Ardhi,basi sheria hiyo ya kimila itakuwa batili.

Kutokana na kuwepo kwa sheria hiyo ndipo Shirika lisilo la kiserikali la Inter Religious Vicoba – IR VICOBA SINGIDA (SIRVICONET) linalojishughulisha na utoaji wa elimu kwa wanawake wa Manispaa ya Singida kwa lengo la kuwafanya wanawake katika Manispaa hiyo kutambua haki zao za msingi juu ya umiliki wa Ardhi kwenye maeneo yao.

Mtandao huo wa IR VICOBA ambao hivi sasa umetimiza umri wa miaka miwili tangu kuanzishwa kwake ni Muungano wa vikundi vya Vicoba vilivyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida.

Lengo kuu la Mtandao huo ni kushirikiana na serikali pamoja na wadau mbali mbali,kujishughulisha na utoaji pia wa elimu kwa jamii katika masuala ya ujasiriamali,elimu ya mazingira na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Malengo mengine ni kutoa elimu ya uraia na utawala bora, masuala ya kupinga ukatili wa wanawake na watoto juu ya masuala ya haki na sheria,ugonjwa hatari wa UKIMWI pamoja na kuwa na sauti ya pamoja katika kuanzisha na kuwa na miradi ya pamoja.

Katika Makala haya Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa SIRVICONET Singida,Lilian Mrua anaelezea changamoto zilizokuwa zikichangia watoto wa kike kutokuwa na haki ya kurithi eneo la Ardhi kama alivyoongea na Mwandishi wa Makala haya,Jumbe Ismailly wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika hilo na kufadhiliwa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la The Foundation For Civil Society.

Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa SIRVICONET Singida anasema idadi kubwa ya wanaume wa Manispaa ya Singida bado wanaonekana kuwa ndiyo wamiliki wakubwa wa ardhi kutokana na sababu mbali mbali.

Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Singida,Bwana Tumaini(wa kwanza kushoto) akipitia mada za kufundisha kwenye mafunzo siku tatu yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano Kituo cha Walimu Nyerere,mjini Singida.

Anazitaja baadhi ya sababu zinazochangia kuwepo kwa idadi kubwa ya wanaume wanaomiliki Ardhi kuwa ni pamoja na mila potofu na desturi za jamii husika,mifumo au taratibu ambazo zipo na mapokeo au desturi.

Kuhusu mila zilizopo  Manispaa ya Singida kuhusu mgawanyo wa mali ikiwemo Ardhi,Mrua anabainisha kwamba kwa kiasi kikubwa mila za hapa zinamkandamiza mwanamke na kumyima haki ya kumiliki Ardhi (mwanamke hathaminiwi).

Akizungumzia makabila yaliyopo katika Mkoa wa Singida kama wazazi wao wanatoa urithi wa Ardhi kwa watoto wao wa kike,Makamu huyo anasisitiza kuwa makabila ya Mkoani hapa,wazazi hawawapi watoto wao wa kike urithi wa  Ardhi kutokana na tabia iliyojengeka kwamba mtoto wa kike ni mpita njia kwa maana kuwa ataolewa kwenye ukoo mwingine,mila na desturi zilizopitwa na wakati,mila kandamizi ambazo wanatakiwa kuziacha.

Naye Mwezeshaji wa mafunzo yanayolenga kupiga vita mila kandamizi kwa mwanamke,Lilian Msasi anasema kwamba kati ya zaidi ya wananchi 16,000 waliopo Manispaa ya Singida, inakadiriwa kuwa takribani asilimia sabini ya wanaume  wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida ndiyo wanaomiliki Ardhi huku asilimia 30 iliyobakia ndiyo inayomilikiwa na wanawake.

Anafafanua kuwa Manispaa ya Singida bado haijatunga sheria ndogo zinazoweza kuwasaidia wanawake wa Manispaa hiyo kupatiwa haki zao wanapokuwa wakizitafuta haki hizo.

Hata hivyo Liliani anaweka bayana kuwa sheria wanazotumia katika Manispaa hiyo ni zile zinazotumika mijini,sheria za Mahakama na sheria ambazo zinaeleza juu ya masuala ya Ardhi na zinatoa haki na fursa sawa kwa wanaume na wanawake kumiliki ardhi.

Kuhusu changamoto zinazojitokeza,mtaalamu huyo wa Mipangomiji anazitaja kuwa ni pamoja na idadi kubwa ya wateja wanaowapata kuwa ni wanaume na kwa upande wa wanawake ni kwamba hawana mwamko na siyo kwa sababu ya kuombwa rushwa,bali wao wanapata pingamizi za kumiliki Ardhi

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mafunzo hayo ya siku tatu yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo cha walimu Nyerere mjini Singida,Ally Jumanne Misanga anasema asilimia kubwa ya wanawake bado hawajui haki zao za msingi za umiliki wa Ardhi,hivyo ni wachache waliomiliki Ardhi hiyo.

Anasema Misanga ambaye pia ni diwani wa kata ya Mwankoko kwamba mila ya kabila la wanyaturu ilikuwa haimpi mtoto wa kike haki ya kumiliki Ardhi na kwamba ni kwa karne ya leo kwa vile watoto wa kike wamepata elimu na kuweza kujua wana haki hiyo ndiyo maana wameanza kudai na kumiliki Ardhi.

Kuhusu wazazi kama wanawapa urithi wa Ardhi watoto wao wa kike kwenye maeneo yao,Mwenyekiti huyo wa mafunzo anaweka bayana kuwa kwa maisha ya sasa watoto wa kike wanapewa haki ya vipande vya Ardhi kuvimiliki.

Akitoa maoni yake wakati wa mafunzo hayo,Afisa mtendaji wa Mtaa wa Kititimo,Rashidi Shang’a anafafanua kuwa umiliki wa Ardhi katika eneo lake upo kwa mujibu wa sheria Namba 4 ya mwaka 2009 pamoja na umiliki wa kimila.

Anasema Shang’a kwamba katika umiliki wa Ardhi kwa mujibu wa sheria namba 4 ya mwaka 2009,uwiano kati ya wanaume na wanawake anaweza kusema kuwa ni asilimia 50 kwa 50 kwa sababu wote wana haki sawa ya kumiliki ardhi.

Anafafanua kuwa katika umiliki wa kimila jamii inamiliki Ardhi hiyo tokea enzi za mababu na mabibi kwa maana hiyo umiliki wake unatawaliwa na wanaume.

Anabainisha pia kwamba mila za eneo lake hilo bado zina dhana ya kuwa mwanamke hawezi kumilikishwa Ardhi kwa kuwa muda ukifika ataolewa na kwenda kupata ardhi kwenye ukoo wa mumewe.

Anasema kulingana na elimu ya kupinga mila zilizopitwa na wakati kwa sasa wazazi wanatoa urithi kwa watoto wa kike sawa na watoto wa kiume na hivyo wazazi wanatoa urithi wa Ardhi kwa watoto wa kike pia.

Afisa mtendaji wa Kata ya Unyambwa,Ruthi Mtinda anasema uwiano wa umiliki wa Ardhi kati ya mwanamke na mwanaume katika eneo lake unaonyesha kuwa wanaomiliki Ardhi kwa asilimia kubwa ni wanaume na kwa kidogo sana kaya zinazoongozwa na wanawake ambao labda waume zao walifariki.

Aidha anasema mila za huko zinamnyima haki mtoto wa kike kwa sababu ni mtu wa kuolewa,hivyo hana haki ya kumilikishwa Ardhi na wanaamini kwamba atapata huko atakakokwenda kuanzisha familia yake.

Akizungumzia sababu za kuwepo kwa idadi kubwa ya wanaume kuwa ndiyo wamiliki wakuu wa Ardhi,Mtendaji huyo anafafanua kuwa wanaume wengi sana ni watu wanaopenda kuona wao ndiyo wanaostahili zaidi kuwa wamiliki wa Ardhi kwa sababu wanadhani mwanamke hawezi kwa sababu ni dhaifu,hana uwezo wa kumudu kusimamia majukumu ya Ardhi.

Akitoa taarifa ya utendaji wa Mradi huo wa IR VICOBA SINGDA,(SIRVICONET),Mratibu wa Mtandao huo katika Manispa ya Singida,Happy Francis anasema kuwa lengo la kuanzishwa kwa mtandao huo ni kushirikiana na serikali pamoja na wadau mbali mbali kutoa elimu kwa jamii katika masuala ya ujasiriamali,elimu ya mazingira na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Afisa Maendeleo ya jamii Manispaa ya Singida,Severina Kilala akifunga mafunzo ya siku tatu ya majukumu ya Mabaraza ya Ardhi,Haki za Umiliki wa Raslimali Ardhi kwa wanawake yaliyofanyika katika ukumbi wa Kituo cha walimu Nyerere,mjini Singida,

“Mradi wa Mtandao wa Inter Religious Vicoba (IR VICOBA) uliopo katika Manispaa ya Singida umeanza kutoa mafunzo ya kuwawezesha wanawake kufahamu haki zao za kutumia na kumiliki rasilimali Ardhi kwa Madiwani,watendaji,wawakilishi wawili kutoka katika mabaraza ya kata,maafisa maendeleo ya jamii na viongozi wa mtandao wa vicoba”anafafanua Happy.

Mafunzo hayo  yaliyofanyika kwa siku mbili kwenye ukumbi wa mikutano wa kituo cha walimu cha Nyerere mjini Singida yalihudhuriwa na washiriki 34 kutoka katika kata tano za Unyamikumbi,Kisaki,Unyambwa,Mwankoko na Mungumaji.

Hata hivyo Mratibu huyo anasisitiza kwamba utafiti uliofanyika ulibaini kwamba asilimia 75 ya familia nyingi katika Mkoa wa Singida wanawake ndiyo wanaohusika katika kazi za kuhudumia na ushahidi ni idadi iliyopo katika vikundi vya VICOBA kwani ni robo tatu ya wanavicoba wote.

Anabainisha Mratibu huyo wa Mtandao wa IR.VICOBA (SIRVICONET) kwamba kwa kuwa wanawake ndiyo wanaohangaika kupata uhakika wa chakula kwa familia,hivyo wameona kuna haja kubwa kwa jamii kupata elimu ya umuhimu wa mwanamke kumiliki raslimali Ardhi ili kuondoa kabisa ile mitizamo hasi kuwa mwanamke hana haki katika umiliki wa Ardhi.

Aidha Happy anasema mradi huo wa kuwezesha wanawake kufahamu haki ya kumiliki Ardhi utatekelezwa katika  kata tano zilizopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida na anazitaja kata zitakazonufaika na mradi huo kwa kipindi cha miezi sita kuanzia august,2017 hadi januari,2018 ni Kisaki,Mungumaji,Mwankonko,Unyambwa na Unyamikumbi

Wakichangia mada ya sheria ya Ardhi baadhi ya wajumbe wa Mabaraza ya kata walielekeza shutuma zao kwenye Mahakama za Ardhi na Nyumba za wilaya kuwa ndizo chanzo kikuu cha haki za wananchi kupotea kutokana na watu wanaotumia fedha kubadili hukumu zinazotolewa na mabaraza ya kata.

Mmoja wa wajumbe wa Baraza la Kata ya Mungumaji,Salumu Yusufu Sife anasema pamoja na wajumbe wa mabaraza ya kata kuwa na ufahamu mkubwa wa maeneo wanakozaliwa,wanakoishi wadai na wadaiwa unaowawezesha kuwapata kwa urahisi,lakini bado wamekuwa wakikandamizwa na kulazimishwa na Mahakama ya ngazi ya wilaya kubadili maamuzi waliyoyatoa.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la kata ya Mungumaji,Shabani Sungi anasema kwamba wajumbe wa baraza la kata hiyo wamekuwa wakikwamishwa kufanyakazi zao kwa mafanikio na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya kutokana na kuzuiwa kutoa haki kwa wadai na badala yake wanalazimishwa kudhulumu haki za wahusika hao.

“Lakini unapotaka kutoa haki unaambiwa na mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya baada ya mtu kwenda huko unaambiwa upeleke jalada la shauri hilo na mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya wapo tayari kula kuliko kufanyakazi”anasisitiza Sungi ambaye ni mwenyekiti wa baraza la kata ya Mungumaji.

Naye Mkuu wa wilaya ya Singida,Eliasi Tarimo akizungumza wakati wa ufunguzi wa kuzindua na kuutambulisha mradi wa kuwawezesha wanawake kumiliki Ardhi,uliofanyika mjini Singida anaviagiza vyombo vinavyoshughulikia utoaji wa haki katika mashauri ya Ardhi,yakiwemo mabaraza ya Ardhi ya vijiji,kata na hata wilaya kujenga utamaduni wa kutoa haki kwa wahusika ili kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima kati ya walalamikaji na walalamikiwa.

Aidha Tarimo ambaye alionekana kutoridhishwa na huduma zinazotolewa na taasisi hiyo nyeti,anabainisha kwamba endapo kama angekuwa na mamlaka hangesita kuyafuta kabisa mabaraza hayo ili yasiendelee kuwepo huku yakidhulumu haki za wananchi na hususani wanawake wajane.

Kwa mujibu wa Tarimo ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzzi na usalama wa wilaya hiyo,mabaraza ya Ardhi katika ngazi zote hayawatendei wananchi  haki hususani kwa wanawake wajane jambo ambalo linaweza kuchangia migogoro kati ya pande mbili zinazoshindana.

“Mabaraza ya Ardhi hayatendi haki nilishawahi kusema ningekuwa mwenye mamlaka ningeyafuta haya mabaraza kwa sababu sehemu nyingi yamekuwa hayatendi haki na sijui ni kwa nini hayabadiliki,utatoa elimu,utaelekeza lakini bado,bado,bado kinachofanyika kwenye yale mabaraza ni magumashi.”anasisitiza huku akionyesha kukerwa na huduma zitolewazo na mabaraza hayo.

washiriki wa mafunzo ya siku tatu ya Majukumu y Mabaraza ya Ardhi  Haki za Umiliki wa Raslimali Ardhi kwa wanawake yaliyofanyika katika Kituo cha Walimu Nyerere,mjini Singida.

Share:

Leave a reply