Taarifa ya BASATA kuhusu kutofanyika fainali za Miss Tanzania 2017

418
0
Share:

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limekua likifuatilia kwa umakini mwenendo wa shindano la Miss Tanzania na waandaji wake kampuni ya LINO Agency katika kuhakikisha taratibu, kanuni na miongozo ya kuendesha matukio ya Sanaa  nchini inazingatiwa.

Hivi karibuni LINO wametoa taarifa ya kutokufanyika kwa shindano Miss Tanzania kwa mwaka 2017 ambapo pamoja na sababu ya kukosa wadhamini wametaja kucheleweshewa kibali na BASATA kama sababu ya kutokufanyika kwa shindano hili kwa msimu wa mwaka 2017.

Tunapenda kueleza kwamba sababu inayotolewa na LINO kwamba walicheleweshewa kibali na BASATA si ya kweli na pengine imetengenezwa kuficha uhalisia wa changamoto za shindano hili ambazo mara zote BASATA na hivi karibuni Waziri mwenye dhamana na sekta ya Sanaa Mh. Dkt Harrison Mwakyembe amezieleza na kuzitolea maagizo.

BASATA kama mtoa vibali vya matukio ya Sanaa nchini limeshangazwa na taarifa ya kutokuwepio kwa shindano kwa msimu huu maana tayari lilikwishatoa kibali cha muda kwa kampuni ya LINO ili kufanya maandalizi ya awali ya shindano hili sambamba na kuandaa mshiriki wa shindano la Miss World 2017 lililomalizika hivi karibuni mji wa Sanya nchini China ambapo Tanzania tuliwakilishwa na mshiriki Julitha Kabete aliyekabidhiwa bendera chini ya uangalizi wa Wizara na BASATA.

Kibali hicho cha muda ambacho kilitolewa mapema tarehe 08/09/2017 kinatoa fursa kwa mwandaaji wa tukio la Sanaa kufanya maandalizi yote ya awali ya tukio la Sanaa/Burudani huku akiwa chini ya uangalizi maalum wa kukamilisha taratibu mbalimbali za msingi kwa ajili ya kupewa kibali cha mwisho cha tukio husika hivyo kampuni ya LINO haina sababu yoyote ya kutaja kibali cha BASATA kama kikwazo cha kufanyika kwa shindano la Miss Tanzania mwaka huu maana tayari walikua na kibali hiki cha muda kinachowapa fursa za maandalizi yote ya awali ya shindano

Tunazidi kutoa wito kwa waandaaji wote wa mashindano/matukio ya Sanaa kuzidisha weledi na zaidi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kuendesha matukio ya Sanaa kama zinavyo fafanuliwa katika vikao vya mashauri mara kwa mara. Aidha tunazidi kusisitiza umuhimu wa kujenga taswira chanya kwa matukio ya Sanaa na kuyajengea uendelevu ili kuvutia wawekezaji zaidi na kuyapa mvuto mkubwa wa kibiashara.

BASATA kama msajili na mtoa leseni katika matukio ya Sanaa tutaendelea kuzingatia weledi na kutoa huduma zetu kwa haraka, ubora na kuzingatia kwa umakini mkubwa sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji matukio ya Sanaa ambazo kwa pamoja wadau wote tumeziridhia.

KATIBU MTENDAJI

BARAZA LA SANAA LA TAIFA – BASATA

Share:

Leave a reply