TAFU yatoa siku 30 kwa wavuvi kusalimisha zana haramu

289
0
Share:

CHAMA  cha wavuvi Tanzania (TAFU) chenye makazi yake jijini Mwanza, kimetoa siku 30 kuanzia sasa wavuvi wote  haramu kusalimisha zana zao ndani ya kipindi hicho, atakayekaidi atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Chama hicho kimedai kitaanza wakati wowote  ‘operation’ maalum  kuwakamata  wavuvi haramu na wataanzia kwenye mabwawa ya Kinyangiri, Kindai na Singidani mkoani Singida, kwa madai uvuvi haramu umekithiri.

IMG_2230

Mvuvi katika bwawa la Kindai manispaa ya Singida,Mzee Salumu Kikomeko (84), akionyesha moja ya vyandarua vya mbu zinazotumiwa na wavuvi haramu katika bwawa hilo.Matumizi ya vyandarua katika uvuvi ni kinyume na sheria za uvuvi.(Picha na Nathaniel Limu).

Onyo hilo limetolewa na Mwenyekiti TAFU Benjamini Mashimba, wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Singida kwenye ukumbi wa mikutano Stanley ya Motel mjini hapa.

Alisema pia watu wanaodhamini wavuvi haramu waache mara moja tabia hiyo, kwa vile  ina madhara makubwa kwa binadamu na viumbe vyote vinavyoishi majini zikiwemo samaki.

“Hawa wavuvi haramu na wadhamini wao,tunawafahamu vizuri mno,kwa hiyo hatutawasaka,tunaenda kuwakamata moja kwa moja”,alisema kwa kujiamini.

Hata hivyo,Mashimba alisema anaimani muda mfupi ujao, uvuvi haramu utakuwa ni historia kutokana na sheria mpya ya sekta ya uvuvi.

Amedai kwamba  sheria hiyo  imekipa nguvu au meno  chama chao,kudhibiti uvuvi haramu ambao unatishia kutoweka samaki na viumbe vingine vinavyoishi majini.

“Tukiendelea kuvumilia uvuvi haramu, pamoja na madhara yake mengi, mbaya zaidi maji yote kwenye bahari, maziwa na mabwawa, yatakuwa yamejaa  sumu inayotumika kwenye uvuvi haramu. Hatutakubali kwa sababu lengo letu ni shughuli ya uvuvi iendelee kuajiri Watanzania wa kizazi cha sasa na kile kijacho”,alisema na kuongeza;

“Sheria ya zamani namba 22 ya mwaka 2003 ilishindwa kusimamia kikamilifu sekta ya uvuvi. Hii ya sasa ambayo mvuvi haramu akipatikana ni hatia, atapewa adhabu ya kulipa faini kati ya shilingi milioni tano na ishirini au kifungo jela mwaka mitano  au adhabu zote mbili”.

IMG_2845

Mwenyekiti wa chama cha wavuvi Tanzania (TAFU) (wa tatu kulia),akizungumza na waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya kuanzishwa kwa operation maalum kuwakamata wavuvi wote haramu nchini.(Picha na Nathaniel Limu).

Aidha, mwenyekiti huyo alisema wamefurahi kupata Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mh. Mwigulu Nchemba, kwa madai ameonyesha dhamira ya kweli ya kufanya kazi na wavuvi wanaozingatia sheria.

Alisema wanaamini chini ya Waziri Mwigullu,lengo la Chama chao kwamba shughuli ya uvuvi inayoajiri Watanzania wengi, itakuwa endelevu na itaendelea kutoa fursa zaidi kwa Watanzania kujiajiri.

Alisema lengo hilo litafikiwa tu ambapo uvuvi haramu utakomeshwa.

“Naomba nitumie fursa hii kuagiza  kuwa wavuvi wote wanaozingatia sheria, washiriki kikamilifu kutokomeza  uvuvi haramu katika maeneo yao.Pia  amewataka wavuvi kujiunga kwenye vikundi na kuvisajili, ili kujijengea mazingira mazuri ya kupata misada mbalimbali ikiwemo kukopesheka na taasisi za kifedha”,alisema.

Kwa upande wake TAFU,kilipendekeza adhabu kwa wavuvi haramu wanao vua kwa sumu,mabomu,baruti,timba na kokoro la kuvuta kwenye maji mafupi,iwe kifungo cha miaka 30 jela au maisha.

Kwa makosa mengine, adhabu iwe faini ya shilingi 30,000 au jela miezi sita au vyote kwa pamoja.

Share:

Leave a reply