Tamasha la Majimaji Selebuka kufanyika Mei 28-Juni 4 mwaka huu mjini Songea

236
0
Share:

Tayari  maandalizi ya tamasha la Majimaji Selebuka ambalo kawaida hufanyika mjini Songea kila mwaka yamepamba moto na waandaaji wamesema kila kitu kinakwenda kwenye msitari huku likisubiriwa kwa hamu  kutimua vumbi kuanzia hapo Mei 28 mpaka Juni 4, mwaka huu mkoani Ruvuma  huku michezo mbalimbali na maonyesho ya biashara za wajasiriamali ikitarajiwa kuwa kivutio.

Tamasha hilo linaandaliwa na kampuni binafsi ya Tanzania ya Mwandi ikishirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Songea Mississippi (So-Mi) ambalo linahusika na mambo ya maendeleo ya jamii kwa wanasongea kwa ushirikiano kati ya Songea Tanzania na Jimbo la Mississippi, Marekani. Tamasha hilo lilianzishwa 2008.

Mratibu wa tamasha hilo, Reinafrida Rwezaura, amesema kuwa hii ni mara ya pili kufanyika kwa tamasha hilo ambapo kwa mwaka huu litahusisha zaidi mambo sita kwa muda wa siku saba huku lengo kubwa likiwa ni kuinua vipaji na fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wakazi wa mkoa huo.

 Rwezaura alisema kuwa tamasha hilo ambalo litafunguliwa kwa mashindano ya mbio za nyika (marathon) katika siku ya ufunguzi huku siku ya mwisho likihitimishwa kwa mchezo wa mbio za baiskeli ambapo washindi wake watapata nafasi ya kwenda nchini Rwanda kwa ajili ya mafunzo ya mbio za kimataifa.

“Tunafanya tamasha hili kwa mwaka wa pili malengo yakiwa ni kuibua vipaji na kuviendeleza kupitia michezo ya mbio za nyika, kuanzia Kilomita 24, 21, 10, 5 mbio za kujifurahisha, pia mbio za mchezo wa baiskeli ambazo tunaamini kwa mwaka huu ni za aina yake kwa sababu tunategemea kupata washiriki kutoka nje ya nchi kama Rwanda.

 “Lakini lengo lingine ni kuibua na kutambua fursa za kiuchumi hasa kwa wajasiriamali wa Mkoa wa Ruvuma kupitia maonyesho ya shughuli za  wajasiriamali pamoja na biashara katika viwanja vya makumbusho ya Vita vya Majimaji.

“Pia tamasha linalenga kuendeleza elimu kwa kufanya mdahalo wa shule za sekondari kupitia wanafunzi wa shule mbalimbali wa ndani na  nje ya Mkoa wa Ruvuma  na kuibua fursa za kitalii,” alisema Rwezaura.

Ada ya ushiriki wa tamasha hilo, kwa mbio za nyika kilomita 42 ni Sh 10,000, kilomita 21 Sh 5,000, kilomita 10 Sh 3,000, kilomita 5 ni bure.

Kwa upande wa mbio za baiskeli kilomita 50 Sh 10,000, ngoma za asili kwa kila kikundi ni Sh 10,000 huku maonyesho ya ujasiriamali kwa kila kikundi ni Sh 50,000 na kwa mtu mmoja ni Sh 10,000.

reinfrida selebukaMratibu wa tamasha hilo, Reinafrida Rwezaura, (Wa pili kutoka kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (Hawapo pichani) wakati wa utambulisho wa tamasha hilo hivi karibuni. (Picha kwa Hisani ya blogu ya Salehjembe).

IMG_7096 copy

Share:

Leave a reply