Tamasha la Sauti za Busara kuja na fursa kibao, 8-11 Februari

133
0
Share:

Kila mwaka katika mwezi Februari, maelfu ya mashabiki wa muziki kutoka katika kila pembe ya dunia wanakusanyika katika eneo la Ngome Kongwe, Mji Mkongwe kuonja ladha ya kipekee ya muziki wa Kiafrika katika Tamasha la Sauti za Busara.

Tamasha hili hutoa fursa nyingi, kwani miafaka ya kibiashara hufikiwa, ushirikiano wa haina tofauti huanzishwa, fani mbalimbali hupata fursa ya kupiga hatua za juu zaidi, na vipaji mbalimbali hupata fursa ya kuonekana kwa mapromota mbalimbali wa matamasha ya kimataifa wanaohudhuria. Kwa mwaka huu tamasha hilo linatarajia kufanyika mwezi ujao yaani Februari 8-11,2018.

“Tamasha hili ni sehemu ambapo watu wenye weledi wa sanaa mbalimbali hukutana, kuanzia kwa wakurugenzi wa matamasha mpaka kwa wazalishaji wa muziki, mameneja wa wanamuziki, wasambazaji wa muziki, wote hawa huja hapa Zanzibar mwezi Februari kushuhudia utamu wa midundo ya muziki wa Ukanda wa Afrika Mashariki,” anasema Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara, Yusuf Mahmoud.

Anaongeza: Hili siyo tu tukio ambalo watumbuizaji pekee huhudhuria, bali hata wanamuziki ambao hawapo katika orodha ya kutumbuiza huja kwa minajili ya kujifunza kutoka kwa wale wanaofanya maonesho mbalimbali, na pia hupata fursa ya kufahamiana na wadau muhimu wa tasnia yao na kutengeneza mahusiano ya kikazi kwa siku sijazo baada ya tamasha kuisha.

Likisifika kuwa miongoni mwa matamasha yenye heshima, Sauti za Busara likiwa na kauli mbiu ya “Kuunganishwa na Muziki” kwa mwaka huu, linawakutanisha pamoja zaidi ya wanamuziki 460 Zanzibar.

Likiwa lina adhimisha miaka 15 tangu lianzishwe Tamasha hili linavutia wataalamu wa habari na muziki kutoka katika kila pembe ya Afrika, Ulaya na mahali pengine, na linatoa jukwaa la kipekee kwa wanamuziki wa Afrika Mashariki kuutanganza muziki wao duniani.

“Kila mwaka, wasani wanaopata fursa ya kutumbuiza katika jukwaa la Sauti za Busara, hualikwa katika miji mbalimbali duniani na kufanya maonesho kwenye matamasha yanayofanyika katika nchi hizo. Wanamuziki ambao hupata fursa ya kualikwa aghalabu, ni wale ambao wamethibitika katika maonesho yao kuwa wabunifu, wenye kuzungumza ujumbe fulani, na wanaocheza muziki wenye utambulisho fulani,” anasema Yusuf.

Kwa mfano Msafiri Zawose, Jagwa Music, Leo Mkanyia, Tausi Women’s Taarab na Maulidi ya Homu ya Mtendeni ni mifano ya vikundi vya Kitanzania ambavyo tayari vimekwishaitwa katika safari za kimataifa baada ya kuonekana katika Tamasha la Sauti za Busara.

Kulingana na maelezo ya Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara, Yusuf Mahmoud, Tamasha la Sauti za Busara ni fursa adhimu ambayo wanamuziki kutoka Tanzania hawatakiwi kukosa, kwa kuwa fursa kama hizi ni chache na ngumu kupatikana Afrika.

“Watu wa rangi tofauti huungana kwa pamoja kusheherekea muziki wa Kiafrika. Matarajio na msisimko ni mkubwa, hoteli zinazopatikana Stone Town huwa zinajaa katika wiki ya tamasha zikiwahudumia watu wanaotoka katika kila kona ya Tanzania, Afrika na Ulaya,” anasema Yusuf.

Kwa makadirio ya haraka, tamasha linachangia kiasi cha $ 7 milioni katika uchumi kila mwaka, kikiwa ni kipindi cha mavuno kwa biashara nyingi zinazofanyika Zanzibar na sehemu zingine, na kulifanya Tamasha la Sauti za Busara kuwa zaidi ya ‘Tamasha la Muziki’.

Hata hivyo, licha ya kuwa na mafanikio hayo yote, changamoto kubwa inayoikumba tamasha hili ni ufadhili, na ndiyo sababu hata tamasha la mwaka 2016 lilifutwa na kusababisha hasara kubwa sana kwa biashara nyingi visiwani Zanzibar.

“Tunaendelea kutegemea fedha za wahisani kutoka katika balozi mbalimbali, ambapo balozi za Norway na Uswisi zikiwa miongoni mwa wafadhili wakubwa, zikisaidia mafunzo na jitihada za ujengaji uwezo,” anasema Yusuf Mahmoud.

Tamasha la Sauti za Busara 2018 linafadhiliwa na Ubalozi wa Norway, Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania na Zambia, Africalia, Mozeti, Zanlink, Memories of Zanzibar, Zenj FM, Chuchu FM, Tifu TV, Music In Africa, Ikala Zanzibar Stone Town Lodge, Emerson Zanzibar, Coastal Aviation, 2Tech Security, Ubalozi wa Ujerumani, Golden Tulip Dar City Centre na wengine wengi.

Na Andrew Chale

Share:

Leave a reply