Tanzania kushirikiana na Oman kuwezesha maendeleo ya biashara

215
0
Share:

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kushirikiana katika nyanja za Kiuchumi, Utamaduni na Ulinzi na Serikali ya Oman ili kuwezesha maendeleo ya biashara baina ya nchi hizi mbili pamoja na Pwani ya nchi za Afrika Mashariki.

Akizungumuza Jijini Dar es Salaam leo wakati alipokutana na ujumbe wa Mfalme wa Oman Sheikh Sultan Qabous Bin Said, Makamu wa Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa ugeni huo ni aina yake kwani utaimarisha masuala ya biashara kwa nchi za ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki.

Katika mazungumzo hayo ambayo yalifanyika katika meli maalum ya Oman iitwayo Fulk Al Salamah na kuambatana na chakula cha mchana, ujumbe wa Oman uliongozwa na Waziri wa Mafuta na Gesi wa nchi hiyo Dkt. Mohammed Hamed Al- Rumhi.

“Huu ni ujumbe maalumu kutoka kwa Mfalme wa Oman ambaye ametuma salamu maalum za ushirikiano kwa wananchi wa Tanzania na nchi za Afrika Mashariki na sisi tunaupokea ugeni huu na kujipanga kushirikiana na Serikali ya Oman katika nyanja za kiuchumi, kiutamaduni na ulinzi na usalama kwa nchi za Pwani ya Afrika Mashariki,” alisema Mhe. Suluhu.

Aidha ameishukuru Serikali ya Oman kwa kuonesha utayari wake wa kufanya kazi na nchi ya Tanzania pamoja na ukanda wa Pwani ya Afrika Mashiriki na kuuhakikishia ujumbe huo kuwa Tanzania na nchi za Pwani ya Afrika Mashariki zitaendelea kushirikiana Oman.

Makamu wa Rais alibanisha kuwa Tanzania na Oman ni marafiki wa muda mrefu na nchi mbili hizo zimesaini mikataba mbalimbali ya ushirikiano ambapo aliahidi kuendelea kuifanyia kazi.

“Siyo mara ya kwanza kwa serikali ya Oman kuja Tanzania kuna mikataba kadhaa ambayo inaimarisha uhusiano hususani kwenye biashara na uwekezaji kwa hiyo ugeni huu ni muhimu kwa nchi yetu,” alisisitiza Mhe. Suluhu.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili ya Utali Dkt. Hamis Kigwangala alisema kuwa ugeni huo kwa Wizara hiyo utatoa fursa ya kujifunza kwa kuangalia Serikali ya Oman inafanya nini ili kuweza kuimarisha Sekta ya Utalii nchini.

“Tumekuja kuangalia na kujifunza wenzetu wanafanyaje katika mbinu za sekta ya utalii kwa mfano serikali ya Oman ina tembelewa na watalii zaidi ya milioni 3.2 kwa mwaka lakini kwa Tanzania sisi tunatembelewa na watalii milioni 1.2, kwa hiyo ugeni huu utaimarisha ushirikiano wa pamoja na Oman katika sekta hii,” alisema Dkt. Kigwangala

Aidha Dkt. Kigwangala alisema wataanzisha ushirikiano wa mradi wa watalii kuja moja kwa moja kutoka Oman mpaka Tanzania na Pwani ya nchi za Afrika Mashariki.

Naye Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani alisema kuwa ujio wa ugeni huo kutoka Oman ni fursa nzuri ya kufanya utafiti wa maeneo ya mafuta kwani serikali ya Oman ni wazoefu na wajuzi katika masuala ya uchimbaji mafuta.

“Tunatarajia ujio huu utajenga uhusiano mzuri katika hatua za utafiti wa mafuta hapa nchini ili kuweza kujenga uzoefu kwa watafiti wetu na kuwawezesha watanzania kuchimba mafuta bila shida kwa sababu wenzetu ni wazoefu katika eneo hili la kiuchumi,” alisema Dkt. Kalemani.

Aidha Dkt. Kalemani alisema kuwa serikali ya Oman wao watajifunza masuala ya gesi asilia kutoka Tanzania kwa hiyo ugeni huo mkubwa ni muhimu kwa nchi zote mbili.

Na.Paschal Dotto-MAELEZO

Share:

Leave a reply