Tanzania yajipanga kukabiliana na uhalifu wa nyuklia

519
0
Share:

Kamishna Mwandamizi wa Polisi, Hussein Laisseri amesema licha ya Tanzania kutokuwa na matishio ya kihalifu, inajitayarisha kukabiliana na matukio ya uhalifu wa nyuklia, kwa kuwapatia maafisa wa vyombo vya usalama vifaa vya utambuzi wa mionzi hatarishi pamoja na mafunzo ya kudhibiti na kupambana na mionzi hiyo kutoka kwa wahalifu.

Kamishna Laisseri ameyasema hayo leo Julai 28, 2017, wakati akifunga mafunzo maalumu ya Uchunguzi wa Nishati ya Nyuklia na Mionzi, yaliyoandaliwa na serikali kwa kushirikaiana na Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) yaliyoshirikisha wataalamu wa masuala ya usalama 59 kutoka nchi 9 duniani.

Amesema kupitia mafunzo hayo ambapo washiriki wake wamejifunza namna ya ugunduzi, uchunguzi na udhibiti wa mionzi ya nyuklia, maafisa usalama hasa wa mipakani wataweza kudhibiti matukio ya uhalifu yanayotokana na matumizi ya mionzi hasa ya nyuklia.

“Hatuna tishio lolote nchini la uhalifu kwa sasa, lakini huwezi kusema tukio likija ndio ujiandae, tumeona ipo haja kujiandaa ili siku mionzi hatarishi ikiwa katika mikono ya wahalifu tujue tunafanyaje. Wahalifu wanaweza kutokea nchi nyingine kwa haraka kutokana na maendeleo ya teknolojia. Huu ni utayari wa kawaida kwa Jeshi la Polisi,” amesema.  

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Teknolojia ya Nyuklia nchini, Firmi Banzi amesema baada ya mafunzo haya kuisha, serikali inatarajia kupata msaada wa vifa vya utambuzi wa mionzi hatari kutoka katika mashirika mbalimbali ikiwemo Interpol, na kwamba itavisambaza nchi nzima kwa maafisa usalama hasa walioko mipakani.

“Tunahitaji vifaa vya kutosha vya kutambua mionzi ikiwemo ya nyuklia, lakini hivi vifaa vinauzwa bei ghali sana na kwamba serikali yetu kupata vifaa vya kusambaza nchi nzima ni nadra. lakini baada ya mafunzo haya kuisha mashirika ikiwemo la Interpol hutoa vifaa kwa watendaji wa masuala ya usalama walio mpakani mwa nchi,” amesema. 

Mafunzo hayo ya siku tano yalianza Julai 24 mwaka huu jijini Dar es Salaam, ambapo ni mara yake ya kwanza kufanyika hapa nchini. Haya ni mafunzo ya sita kufanyika tangu kuanzishwa kwake.

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply