TASAF yatumia milioni 430 kujenga zahanati nne Singida

306
0
Share:

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mkoa wa Singida, umetumia zaidi ya shilingi 430.3 milioni kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa zahanati nne katika halmashauri za wilaya ya Ikungi, Mkalama, Singida vijijini na Manispaa ya Singida.

Fedha hizo pia zimegharamia ujenzi wa nyumba mbili (two in one) za kuishi walimu katika shule ya msingi Chikombo wilaya ya Manyoni na shule ya Msansao iliyopo wilaya ya Iramba.

Ujenzi wa miundombinu hiyo kupitia TASAF 111 kipengere cha ujenzi wa miundombinu maalum umefanyika kati ya Septemba 2014 na Machi mwaka huu.

Hayo yamesemwa juzi na mratibu TASAF mkoa wa Singida, Patrick Kasango, wakati akitoa taarifa yake ya utekelezaji wa ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Mwahango kata ya Ilongero halmashauri ya wilaya ya Singida.

Alisema pia wananchi wa vijiji vya miradi hiyo, wamechangia zaidi ya shilingi milioni 61.6 kwa kuchangia nguvu zao.

Kasango alisema kabla ya utekelezaji wa miradi hiyo kulifanyika tathimini na uhakiki ili kubaini hali halisi ya uhitaji wa huduma halisi.

“Pia lengo ni kujiridhisha kwamba miradi hiyo kama itaweza kusaidia  walengwa kutimiza msharti ya elimu bora na afya katika mpango wa kunusuru kaya maskini, katika halmashauri sita mkoani kwetu,” alisema.

Kwa mujibu wa mratibu Kasango,kati ya septemba 2014 hadi machi mwaka huu, TASAF 111 mkoa wa Singida imetumia fedha zingine zaidi ya shilingi 23.1 bilioni kugharamia utekelezaji wa kipengere cha uhawilisha fedha (conditional cash Transfer). Jumla ya kaya zipatazo 38,984 kutola halmashauri sita vijiji 277 zimenufaika na fedha hizo.

Aidha, amesema katika programu ya kutoa ajira za muda kwa kaya maskini, zaiidi ya shilingi bilioni 2.7 zimelipwa kwa kaya zilizofanya kazi za muda, ikiwemo ujenzi wa mabwawa ya maji na upandaji miti.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika hafla hiyo,mkuu wa mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi,ametumia fursa hiyo kuuomba uongozi wa mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) makao makuu, kusaidia ujenzi wa nyumba kubwa (two in one) katika zahanati ya Mwahango.

“Binafsi na kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Singida,naishukru sana TASAF 111.Mfuko huu umefanya mambo makubwa na umekuwa mkombozi kwa wananchi kiuchumi. Mkurungezi TASAF makao mkuu, usichoke kutusaidia, wananchi wa kijiji cha Mwahango wapo tayari kushiriki ujenzi wa nyumba ya watumishi, na wewe nakuomba uwaunge mkono kadri uwezo utakapokuruhusu,” alisema Dk.Nchimbi.

Awali afisa mtendaji wa kijiji cha Mwahango, Leonard Muna, alisema jumla ya wakazi wa kijiji hicho, 2,776 watanufaika na huduma za afya zitakazotolewa kwenye zahanati hiyo mpya.

“Kukamilika kwa mradi wa ujenzi jingo la zahanati,kutasaidia wanakijiji kupata huduma za kiafya kwa karibu zaidi na hasa akina mama na watoto. Pia mradi utasaidia kuinua kipato cha wananchi kwa vile huduma zitapatikana kwa kwa ukaribu sana,” alisema Muna.

Na Nathaniel Limu, Singida

Share:

Leave a reply