TBL Group yatoa msaada wa milioni 100 /-kwa waathirika wa tetemeko la ardhi Kagera

255
0
Share:

Kampuni ya TBL Group mwishoni mwa wiki imemkabidhi Waziri Mkuu,Mh.Kassim Majaliwa shilingi milioni 100/- kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Septemba 10 mwaka huu.

Mkurugenzi Mkuu wa TBL Group,Roberto Jarrin,amesema kampuni yake imeguswa na janga hili kubwa hapa nchini ambalo limesababisha vifo vya watu na kubomoa makazi na miundo mbinu na inaungana na wadau wengine kusaidia waathirika ili waweze kurejea katika hali zao za  awali na kuendelea na maisha  yao ya kawaida.

“Tunaunga mkono  jitihada za serikali za kusaidia wahanga wa tukio la tetemeko la ardhi mkoani Kagera.Tupo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu walichonacho wakati serikali inafanya jitihada za kuhakikisha wanaendelea kupata huduma za kijamii ambazo zimevurugwa na janga hili”.Alisema Jarrin.

tbl-kageraMkurugenzi Mkuu wa TBL Group,Roberto Jarrin (kulia) akimkabidhi Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa (wa tatu kutoka kulia) hundi ya shilingi milioni 100/-kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.(Kushoto) ni Mkurugenzi wa Masuala ya Ndani na Nje wa kampuni hiyo,Georgia Mutagahywa na (wa pili kutoka kulia) ni Fabian Mwakatuma –Mkuu wa kitengo cha Ugavi wa TBL Group.

Roberto aliongeza kuwa  moja ya sera ya TBL Group  ni kusaidia jamii inakofanyia  biashara zake wakati wote na ndio maana mbali na kutoa msaada huu wa majanga imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali ya kuleta mabadiliko kwenye jamii hususani katika sekta ya afya,Mazingira na maji,elimu na kilimo.

“Siku zote tutakuwa mstari wa mbele kuunga mkono jitihada za serikali za kuboresha maisha ya wananchi kwa kufadhili miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo kutoa misaada wakati anapojitokeza majanga kwenye jamii.

Kwa upande wake,Waziri Mkuu ,Kassim Majaliwa alishukuru TBL Group, makampuni yote na wadau wengine ambao wameonyesha moyo wa kusaidia wahanga wa tetemeko la ardhi ambao wanahitaji msaada wa kukarabati na kujenga makazi na miundombinu mingine.

Share:

Leave a reply