TFF yaingiza mguu rasmi sakata la Yanga, yamtaka Katibu Mkuu aonyeshe mkataba

215
0
Share:

Taarifa za Yanga kuingia mkataba wa kuikodisha timu kwa miaka kumi kwa Kampuni ya Yanga Yetu zimezidi kuchukua sura mpya ambapo licha ya baadhi ya wanachama wa klabu hiyo kupinga utaratibu uliotumika, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nalo limefunguka kuhusu jambo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa amezungumza kuhusu mabadiliko ambayo wameyafanya na kusema wao kama TFF bado hawajayatambua mabadiliko hayo na wamemwandikia barua Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit ya kumtaka aonyesha mkataba ambao wameingia na kampuni ya Yanga Yetu.

“Nimemuandika barua Katibu Mkuu wa Yanga atupe nakala ya mkataba ule (wa Yanga na Kampuni ya Yanga Yetu), ili kama kuna wasiwasi hilo tatizo lishughulikiwe mapema maana hizi klabu niza wanachama, wanaweza kuingia mikataba na wanachama wengine wakaja na mambo mengine,

“Tunataka mkataba uwe wazi ili hata klabu zingine zijifunze, kwahiyo Yanga tumewaomba walete copy ya huo mkataba nini kinaazimwa na kipi kinauzwa, klabu itaendeshwaje na baada ya hapo kamati za TFF zitakaa kulijadili jambo hilo, kama itakuwa tofauti na kanuni zetu tutarudi kwao warekebishe mambo ambayo hayapo sawa,” alisema Mwesigwa na kuongeza.

“Uendeshwaji lazima ubadilike kuendana na wakati lakini hatutaki mabadiliko yasababishe mvurugano ambao haukuwepo kwa muda mrefu na tumeshapokea barua nyingi za wanachama wa Yanga hadi wazee wamekuja wanasema wanataka kwenda kumwona mkuu wa nchi”

Aidha alisema TFF bado inatambua Yanga inasimamiwa na uongozi wa klabu kama ilivyokuwa awali ikiongozwa na Mwenyekiti, Yusuph Manji na kama kutakuwa na jambo la tofauti watatoa taarifa baada ya kujiridhisha mfumo ambao Yanga itakuwa inautumia kukodisha timu kwa Kampuni ya Yanga Yetu.

Share:

Leave a reply