THBUB watoa tamko la maadhimisho ya siku ya watu wanaoishi maisha ya asili

347
0
Share:

Jana Septemba 13, 2017, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeungana na wadau wa haki za binadamu ulimwenguni kote kuadhimisha miaka 10 ya Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wanaoishi maisha ya asili.

Hii ni kila Septemba 13, 2007 ambapo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio kuhusu haki za watu wanaoishi maisha ya asili ambalo linaainisha mambo mengi kuhusu haki hizo. Azimio hili linatoa mwongozo kwa Serikali na jamii duniani kote kuhakikisha kuwa zinaheshimu, zinalinda na kukuza haki za binadamu za watu wanaoishi maisha asilia, kama zilivyoainishwa katika mikataba ya kikanda na kimataifa.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti THBUB, Mh. Bahame Tom Nyanduga ameabainisha kuwa,  Mwaka huu tarehe ya Septemba 13, dunia inaadhimisha kumbukumbu ya miaka 10 ya Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wanaoishi maisha ya asili. Umoja wa Mataifa, pamoja na Serikali duniani kote zinatakiwa kufanya tathmini ya mafanikio yaliyofikiwa katika kutambua, kukuza, na kulinda haki za watu wanaoishi maisha ya asili, pia changamoto walizokumbana nazo katika utekelezaji wa Azimio hilo.

Ndani ya muongo mmoja uliopita kumekuwepo na changamoto ya kutambuliwa rasmi kwa haki za watu wanaoishi maisha ya asili na utekelezaji wa sera zilizopo na Serikali duniani kote ikiwemo Tanzania. Hivyo, haki za msingi za watu wanaoishi maisha ya asili zimeendelea kutotambuliwa na jamii.

Msimamo wa Serikali ya Tanzania katika kutambua haki za watu wanaoishi maisha ya asili Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni miongoni mwa mataifa 144 ambayo yalipiga kura kuunga mkono Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wanaoishi maisha ya asili. Azimio hili linazitaka nchi wanachama “kukubali na kuchukua hatua za pamoja za kushughulikia hali duni za watu wanaoishi maisha ya asili kulingana na misingi ya haki za binadamu iliyoko ndani ya Azimio hili.”

Licha ya ukweli kuwa Tanzania iliunga mkono Azimio hili, haitambui uwepo wa watu “wanaoishi maisha ya asili” hapa nchini kwa sababu inaamini kuwa “Watanzania wote wenye asili ya kiafrika ni watu wanaoishi maisha ya asili.” Hapa nchini kuna jamii za Wahadzabe na Akiye, ambao ni wawindaji na wakusanya matunda, na Barbaig au Datoga na Wamasai ambao ni wafugaji, ambapo wanakidhi vigezo vya Umoja wa Mataifa vya kutambulika kama watu wanaoishi maisha ya asili na Serikali inafahamu uwepo wao. Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu imetambua makundi haya ya jamii ya watu wanaoishi maisha ya asili.

Nchini Tanzania hakuna sera maalumu ya taifa au sheria inayotambua uwepo wa watu wanaoishi maisha ya asili, wala utekelezaji wa Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wanaoishi maisha ya asili.

Hata hivyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeridhia Mkataba wa Kimataifa kuhusu Bioanuai na mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia  nchi. Katika ngazi ya kitaifa, Serikali imeandaa Rasimu ya Programu ya TASAF awamu ya tatu kuhusu Mfumo wa Sera ya watu wanaoishi maisha ya asili na inatekeleza mradi wa upunguzaji na uondoaji wa hewa chafu kutokana na ukataji miti na utowekaji wa misitu.

Kwa maneno mengine Serikali inatambua, japo siyo moja kwa moja, uwepo wa jamii hizi.

Changamoto zinazowakabili watu wanaoishi maisha ya asili nchini Tanzania. Pamoja na kupitishwa kwa Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu watu wanaoishi maisha ya asili miaka 10 iliyopita, watu wanaoishi maisha ya asili nchini Tanzania wameendelea kukabiliwa na changamoto zifuatazo: Hii ni pamoja na Kutokuwepo kwa sheria maalumu inayowatambua, Ukosefu wa uwakilishi katika vyombo vya maamuzi katika ngazi zote.

Pia suala la kuwa na Huduma duni za jamii, kama vile kutopatikana kwa maji safi na salama, huduma za afya, na vifaa vya elimu katika maeneo wanayoishi, Miundombinu duni kama vile barabara, maeneo ya malisho, mfumo wa mawasiliano, maeneo ya uwindaji na ukusanyaji matunda, Ukosefu wa utekelezaji bora wa mikakati inayolenga kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabia nchi katika maeneo ya makazi yao, Ukosefu wa malisho na uvamizi wa ardhi za makazi yao ya asili kwa shughuli za kiuchumi.

Hivyo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inapendekeza mambo yafuatayo kwa Serikali: “Itunge sheria maalumu inayowatambua watu wanaoishi maisha ya asili na haki zao kama zilivyoainishwa katika mikataba ya kikanda na ya kimataifa ya haki za binadamu.

Iridhie Mkataba Na. 169 wa Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) na iingize vifungu vyake katika sheria za nchi. Ihakikishe uwepo wa mgawanyo sawa wa rasilimali kama vile ardhi na rasilimali nyingine za asili zinazopatikana katika maeneo ya jamii ya watu wanaoishi maisha ya asili.

Iwashirikishe watu wanaoishi maisha ya asili katika upangaji na utekelezaji wa maamuzi juu ya masuala yanayoathiri maisha yao na mwisho Ifanye mashauriano na jamii ya watu wanaoishi maisha ya asili wakati wa upangaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kupata ridhaa yao kabla ya utekelezaji wa miradi hiyo na wakiwa na taarifa za kutosha.” Ilieleza taarifa hiyo ya Mwenyekiti wa THBUB

Mwenyekiti THBUB, Mh. Bahame Tom Nyanduga 

Baadhi ya Wahadzabe wanaopatikana nchini Tanzania wakiwa katika shughuli zao za kutengeneza chakula

Share:

Leave a reply