Tibaijuka apendekeza mpango wa Mwalimu Nyerere utumike kukomesha mafuriko

79
0
Share:

Kufuatia mafuriko yanayotokea mara kwa mara katika Jiji la Dar es Salaam, Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka amesema ili kukomesha mafuriko hayo na athari zake, serikali inatakiwa iboreshe mipango miji, huku akiisisitza kuufanyia kazi mpango wa uboreshaji mipango miji wa Mwalimu Julius Nyerere wa mwaka 1979.

Tibaijuka ametoa ushauri huo kupitia taarifa yake kwa umma aliyoitoa mapema akiwa Bungeni mjini Dodoma, ambapo amesema mpango huo uliofahamika kama The Nyerere Master Plan ulikuwa na lengo la kufanya bonde la mto Msimbazi kama hifadhi ya jiji la Dar es Salaam kwa kuhakikisha nyumba hazijengwi katika bonde hilo.

Ameeleza kuwa, kinachosababisha mafurikio ya mara kwa mara ni uzibaji wa njia za asili za upitaji maji unaosababishwa na kitendo cha kujengwa makazi ya watu katika bonde la mto Msimbazi ambapo bonde hilo hutumika kama njia ya upitaji maji yanayotoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kuelekea baharini.

“Nilipokuwa ardhi nilijitahidi sana kuokoa bonde la msimbazi kwa mujibu wa mpango miji wa 1979, Call it the Nyerere Master plan. Sikufanikiwa. There was no political will for it. Bonde likaendelea kujengwa. Kwa hiyo maji hayana njia za kufika baharini,” amesema na kuongeza.

“Mind you (niwakumbushe) Bonde la Msimbazi ndiyo njia pekee kwa maji yote yatokayo Pugu Hills Ukonga Airport Tazara Tabata Kigogo magomeni Ilala kufika Jangwani grounds hadi salender bridge yanapoingia baharini. Pia maji kutoka ubungo Manzese Tandale magomeni Kagera kinondoni hananasif Muhimbili hadi jangwani njia ni hiyo tu moja.Kwa upande wa chuo kikuu mto mbezi na mto mlalakuwa na mto Mdumbwi ( Kawe) imejengwa na njia za maji kuifikia kuzibwa.”

Prof. Tibaijuka ameongeza kuwa “Mfano katika eneo la Jangwani, tulisema lakini uharaka wa kukamilisha mradi wa DART ukafunika fikra nyingine. Nilisikitika sana kujua ni kichocheo cha maafa lakini mipangomiji ni shughuli za kisiasa, bila msaada wa nguvu za kisiasa, ujuzi na utaalamu wote hupotea, hauwezi kusaidia.”

“Bila nidhamu ya kuheshimu mipango miji mafuriko yatakuwa common feature (hali ya kawaida) ya jiji la DSM. Regrettably (cha kusikitisha) tatizo siyo mvua kubwa. Tatizo ni kuziba natural drainage system (mfumo asili wa mifrereji ya maji )hivyo maji ya mvua kushindwa kwenda baharini,” amesema Tibaijuka.

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply