TTCL kuanza kutoa huduma za kifedha

381
0
Share:

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameitaka Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kujipanga na kuanza mkakati wa kutangaza huduma za fedha ambazo zitatolewa na kampuni hiyo mwanzoni mwa mwaka ujao.

Prof. Mbarawa ametoa agizo hilo baada ya kukagua mitambo itakayotumika kwa huduma hiyo ambayo itaongeza ushindani wa biashara kwenye huduma za simu nchini mkoani Dodoma.

“Lazima mjipange kwenye idara ya masoko kwa kuanza kutangaza huduma hiyo kupitia njia zote zikiwemo mitandao ya kijamii, ili wananchi warahisishiwe huduma za fedha kupitia TTCL”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Aidha, ameiagiza kampuni hiyo kupitia idara ya masoko kujipanga kuona fursa zilizopo kwa kufahamu mahitaji ya wateja wao na  kuhakikisha inaongeza wateja katika mkoa huo ili kuteka soko la ushindani  ambapo Serikali inajipanga kuhamia huko.

1

Mhandisi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Paul Magembe akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, kuhusu mitambo ya kutolea huduma za kifedha iliyopo katika ofisi za Kampuni hiyo mkoani Dodoma.

Waziri Prof.Mbarawa ametaja baadhi ya maeneo ambayo TTCL inahitaji kuboresha zaidi ni upande wa Simu (Voice) na Data (video) ili kuweza  kurahisisha mawasiliano kwa njia ya video conference  kwa kuwa kuna baadhi ya watendaji wengine watabaki Dar es salaam.

“Mkiimarisha mawasiliano  upande wa data mtarahisisha hata maamuzi na pia kazi zitaenda vizuri Serikalini hasa ukizingatia baadhi ya watumishi watakuwa hapa Dodoma na wengine Dar es Salaam”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Sambamba na hilo, Waziri Mbarawa ameliagiza Shirika la Posta nchini kuja na mkakati wa kuandaa matangazo ya  kutambulisha huduma ya Posta mlangoni kwa jamii ili kuiwezesha huduma hiyo kutambulika kirahisi.

2

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akitoa ufafanuzi kwa baadhi ya watendaji wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), alipokuwa akikagua mitambo ya kutolea huduma za kifedha iliyopo katika ofisi za Kampuni hiyo mkoani Dodoma.
 
Amesisitiza kwa Taasisi hizo kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ili kufikia malengo waliojiwekea na kuendana na kasi ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Akiwa mkoani humo Prof. Mbarawa amemhakikishia Mkuu wa Mkoa, Jordan  Rugimbana kuboresha miundombinu nchini hususan katika mkoa huo ikiwemo kuboresha usafiri wa anga katika uwanja wa ndege wa Dodoma ili kuruhusu ndege kubwa kuweza kuruka na kutua.

Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa ameongea na watendaji pamoja na wafanyakazi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara yake na kusisitiza kufanya kazi kwa kasi, uadilifu, ubunifu na kushirikiana katika utendaji wa majukumu yao ya kila siku.

3

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akitoa maelekezo  kwa Meneja wa Shirika la Posta Nchini, kanda ya Dodoma Bw. Laurent Thobias (kulia), kuhusu utoaji wa matangazo ya huduma ya Posta mlangoni katika ofisi za Shirika hilo mkoani humo.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi hao Meneja wa Wakala wa Majengo(TBA) mkoani humo, Arch. Masalu Bururu,  amemuahidi Waziri huyo kutekeleza yale yote aliyowàagiza ili kuleta ufanisi na tija kwa Taifa.

Waziri Prof. Mbarawa amemaliza ziara yake ya siku kumi katika mikoa ya Mwanza, Mara, Arusha, Manyara na Dodoma ambapo ametembelea miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa na Wizara hiyo.

4

Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme Nchini (TEMESA), Mkoa wa Dodoma, Eng. Bikulamchi Liberatus, akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, kuhusu mikakati ya utengenezaji wa magari katika karakana iliyopo Mkoani humo.

5

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akizungumza na watumishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo (hawapo pichani), alipokutana nao Mkoani Dodoma.

6

Baadhi ya Watumishi wa Taasisi za Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, wakimsikiliza Waziri wa WIzara hiyo (hayupo pichani), alipokutana nao kuwapa mikakati ya utendaji wa Wizara hiyo, Mkoani Dodoma,(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi  na Mawasiliano).

Share:

Leave a reply