“Tuachane na hamasa ya mambo ambayo hayana tija kwa taifa letu”- Majaliwa

279
0
Share:

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watanzania kuachana na hamasa ya mambo yasiyo na tija kwa masilahi ya Taifa.

Waziri Majaliwa ametoa wito huo leo Makao Makuu ya Nchi mjini Dodoma katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa-Standard Gauge kutoka Morogoro hadi Dodoma.

“Tuachane na hamasa ya mambo ambayo hayana tija kwa taifa letu, tuhamasishane katika shughuli za serikali. Tanzania siyo ya mifano ya kulinganisha na nchi nyingine, Tanzania sasa ni nchi ya kuigwa, tuendelee kuuunga mkono, kila mmoja tuendelee kumuombea rais na wasaidizi wake ili wafanye kazi vizuri,” amesema.

Vile vile, amewataka watanzania kumlinda Rais John Magufuli, huku akiwasisitiza kumuombea kwa Mungu ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa manufaa ya Taifa.

“Kila mmoja ahakikishe anamlinda rais wetu, miundombinu yetu na maendeleo yetu kwa maendeleo ya Taifa, tunamhakikishia kila analopanga tutasimamia,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Majaliwa amesema serikali haitaruhusu mwanya kwa mtu yeyote atakayeharibu mipango ya rais ya kuleta maendeleo, kwa kuwa mipango hiyo imelenga kuwanufaisha wananchi.

“Hatutaruhusu mwanya kwa yoyote atakayeharibu mipango hii ili kila mmoja yamletee tija katika taifa letu,” amesema.

Na Regina Mkonde

Share:

Leave a reply