Tume ya Utumishi wa walimu yatajwa kuongeza ubora Sekta ya Elimu

347
0
Share:

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imetajwa kuwa kiungo muhimu katika kuwawezesha walimu kutoa mchango wao utakaosaidia kukuza Kiwango cha elimu hapa nchini.

Akizungumza wakati wa ziara ya Ujumbe wa Tume hiyo Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Deogratius Ndejembi amesema kuwa anaipongeza Tume hiyo kwa kuweka mkazo katika matumizi ya TEHAMA.

“Teknolojia ni jambo muhimu sana katika kusaidia kuharakisha maendeleo na kuongeza ufanisi kwa kuondoa udanganyifu unaoweza kujitokeza katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya kuwahudumia wananchi,” alisisitiza Ndejembi

Akifafanua zaidi Mhe. Ndejembi amesema mifumo ya TEHAMA inayoenda sambamba na mahitaji ya ulimwengu wa sasa ni chachu ya maendeleo hapa nchini.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Bw. Audiphace Mushi amesema kuwa Tume imewezesha walimu kutambua haki na wajibu wao,kusaidia walimu kupata haki zao kwa wakati.

Tume ya utumishi wa Walimu imekuwa mhimili muhimu katika kuwasimamia walimu hivyo ni vyema kila mdau akasaidia juhudi za Tume ili kuimarisha utendaji wake.

Tume ya Utumishi wa Walimu imetembelea Wilaya za Chemba, Bahi, Chamwino, Kondoa, Mpwapwa na Kongwa ili kujionea hali halisi ya utendaji wa Makatibu Wasaidizi wa Tume ngazi ya Wilaya hali itakayochochea na kuhamasisha wadau kujitokeza na Kusaidia Tume kukabiliana na changamoto zinazowakabili walimu kote nchini.

Na Frank Mvungi, Dodoma

Share:

Leave a reply