“Tumeongeza Bajeti Kuinua Wajasiriamali”- Waziri Mwijage

161
0
Share:

Waziri Mwijage amejibu hoja mbalimbali zilizoelekezwa katika Wizara yake kwene ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambapo amesema ameshaagiza hatua za haraka zichukuliwe kwa taasisi zote zilizo chini ya wizara yake kutekeleza hoja mahsusi za CAG.

Kwa upande wa hoja ya mchango mdogo wa Sekta ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati nchini, Waziri Mwijage amefafanua kuwa wakati lengo kuu ni ifikapo 2025 sekta hiyo kuchangia Pato la Taifa kwa asilimia 40, tayari kwa ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi, inachangia asilimia 35, ambazo ni kubwa ikilinganishwa na nchi jirani.

“Kwa kulinganisha mchango wa sekta hii kwa Tanzania katika pato la taifa na nchi nyingine bado nchi yetu inafanya vizuri. Kwa Kenya sekta hiyo inachangia takribani asilimia 25, Uganda asilimia 20, Afrika ya Kusini asilimia 36, India asilimia 40 na Malaysia 40,” alisema.

Aidha, Waziri Mwijage amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mageuzi makubwa katika utoaji wa mtaji kwa Mfuko wa Kuendeleza Wajasiriamali (NEDF) na Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo (SIDO) ambapo mwaka jana Mfuko huo ulipewa Bajeti ya Shilingi bilioni tano (5), mwaka huu Bajeti iliongezwa hadi shilingi bilioni saba (7.8).

Bajeti ya SIDO imeongezeka mpaka shilingi bilioni 26.8; kiasi ambacho ni cha kihistoria kwani hakijapata kutolewa na Serikali kabla ya kuingia Awamu ya Tano.

“Kama CAG alivyobaini, sekta hii ni uti wa mgongo wa Taifa kulingana na uchangiaji wake katika pato la Taifa na ajira. Kutokana na nafasi ya sekta hii katika kujenga taifa la uchumi wa kati, ni mpango wa Wizara kuendelea kuiongezea rasilimali zaidi,” alisema.

Katika mfululizo wa Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano kufafanua utekelezaji wa hoja mbalimbali za CAG, Jumatatu ijayo itakuwa zamu ya Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo.

Share:

Leave a reply